Habari Mseto

Ombeta alalamikia masharti makali ya dhamana kwa wateja wake

August 15th, 2018 2 min read

Na RICHARD MUNGUTI

WAKILI Cliff Ombeta anayewakilisha waliokuwa wafanyakazi saba wa zamani wa kaunti ya Nairobi wanaoshtakiwa kwa kashfa ya Sh213 milioni alimkashifu hakimu kwa kuwaachilia kwa masharti makali ya dhamana.

Bw Ombeta alimshutumu hakimu mwandamizi Bw Lawrence Mugambi kwa kukalia faili hiyo na kutowapa dhamana ya pesa tasilimu washtakiwa tisa wanaokabiliwa na shtaka kupelekea kaunti kupoteza mamilioni ya pesa kwa kulipa kampuni mbili za Lodwar Wholesalers Ltd na Ngurumani Traders Limited.

Bw Mugambi alikataa kuwapa dhamana ya pesa tasilimu jinsi aliyekuwa Gavana wa Nairobi Dkt Evans Kidero alivyoachiliwa aliposhtakiwa Alhamisi  wiki iliyopita.

Washtakiwa hao wanakabiliwa na kulipa makampuni ya Ngurumani Traders Limited (NTL) na Lodward Wholesalers Limited (LWL) mamilioni hayo ya pesa kati  ya 2014 na 2016.

Walipojisalamisha katika afisi za EACC Jumatatu asubuhi washtakiwa hao walinyimwa dhamana licha ya hakimu mwandamizi Bw Lawrence Mugambi kuelezwa Dkt Kidero na aliyekuwa afisa msimamizi wa masuala ya fedha Bw Maurice Okere walikuwa wameachiliwa kwa dhamana ya Sh2milioni pesa tasilimu  , dhamana ya Sh3milioni na mdhamini mwingine wa Sh5milioni.

Hakimu mkuu mahakama hiyo ya kuamua kesi za ufisadi Bw Douglas Ogoti aliwakubalia Dkt Kidero kulipa dhamana hiyo ya pesa tasilimu na kutia saini cheti kwamba atailipa Serikali Sh5milioni ikiwa atakosa kufika kortini siku za kusikizwa kwa kesi.

Punde tu baada ya kuwaachilia kwa dhamana wakili Cliff Ombeta anayewatetea washtakiwa hao alieleza kutoridhika kwake na jinsi hakimu aliwanyima dhamana washtakiwa Jumatatu akidai alikuwa na kazi nyingi.

Bw Ombeta alimweleza hakimu kwamba amekandamiza haki za washtakiwa kuwa kukaa na faili hiyo tangu juzi na hatimaye kuwaachilia kwa dhamana mwendo wa saa nane mchana.

“Naomba hii mahakama isome tena vifungu nambari 20 na 21 vya Katiba uhuru na haki za kila mkenya,” alisema Bw Ombeta.

Wakili alimweleza hakimu huyo kuwa kila mmoja anatastahili kupewa haki zake na ni jukumu la kila mtumishi wa umma kuhakikisha wananchi wamepata haki zao.

Saba hao walifiokishwa kortini baada ya kujisalimisha kwa maafisa wa tume ya kupambana na ufisadi nchini EACC walizuiliwa korokoroni hadi jana alasiri walipoachiliwa kwa dhamana.