Habari za Kitaifa

Ombi la kutaka kuzika mwili uliokaa mochari miaka 10 lapingwa

February 28th, 2024 2 min read

NA BRIAN OCHARO

MJANE wa marehemu Harry Roy Veevers aliyekuwa bwanyenye raia wa Uingereza na binti zake wawili, wamepinga ombi la wana wawili wa marehemu kuondoa mwili wake katika mochari ya Mombasa ili wakauzike nchini Uingereza.

Bi Azra Parveen Din na binti zake wawili, Bi Hellen Veevers na Bi Alexandra Veevers, wamepinga pia shinikizo la wana wengine wawili wa marehemu wanaotaka kufunguliwa upya kwa uchunguzi wa kifo cha baba yao.

Richard John na Philip David Veevers walikuwa wameomba korti iwaruhusu kuondoa mwili wa baba yao ambao umekaa katika mochari kwa karibu miaka 10 ili wauzike Uingereza, huku pia wakipendekeza uchunguzi upya kuhusu chanzo cha kifo chake.

Kupitia kwa wakili wao Mogaka Omwenga, mjane huyo na binti zake wawili wameshikilia kuwa mahakama ya hakimu mkazi iliendesha vikao vya uchunguzi kwa haki, huku pande zote na mashahidi wakipewa muda wa kutosha kuwasilisha ushahidi wao.

Aidha, wanadai kuwa Mahakama Kuu pia inaweza kufikia uamuzi sawa na wa mahakama ya hakimu iwapo itaangalia upya kesi hiyo.

“Maombi ya kufungua kesi hiyo yanatokana na uvumi na dhana kwamba Hakimu alilazimishwa kuandika uamuzi huo. Jukumu la Hakimu katika uchunguzi huo lilikuwa kubaini chanzo cha kifo na waliohusika kwa ajili ya kufunguliwa mashitaka,” alisema wakili.

Zaidi ya hayo, wamesema kuwa Hakimu hakuwa na mamlaka ya ziada ya kuchunguza makosa mengine yanayodaiwa dhidi ya mali ya marehemu nchini Kenya au Uingereza na/au dhidi ya watu wengine waliotajwa kwenye nyaraka zilizowasilishwa na Bw Richard na Bw Philip.

“Ombi la Bw Richard kuwa apewe mwili wa marehemu linapaswa kufanywa rasmi katika kitengo kingine cha mahakama ambapo wahusika wote watapewa fursa ya kuwasilisha hati zao na kuhojiwa kabla ya uamuzi kufanywa,” walisema.

Bw Richard na Bw Philip wameomba Mahakama Kuu ifungue upya uchunguzi huo, wakisema mahakama ya hakimu mkazi ilipuuza ushahidi muhimu ambao ungesababisha kufunguliwa mashtaka kwa watu wanaoshukiwa kuhusika katika kifo cha baba yao. Wana hao wawili pia wanataka wapewe mwili huo ili kuurejesha nchini Uingereza kwa ajili ya mchakato mwingine wa upasuaji kabla ya kuzikwa eneo la Rochdale, Greater Manchester.

Bw Richard na Bw Philip pia wamesema kuwa, mwili huo utafanyiwa uchunguzi mwingine mara tu utakapowasili Uingereza.

Kulingana nao, uchunguzi uliofanywa haukuwa tu wa kubaini ni nani aliyemuua baba yao, bali pia kuangalia matukio mengine yaliyofuatia baada ya kifo chake.

Matukio hayo ni kama kukosa kutoa taarifa ya kifo hicho kwa polisi na kuondolewa kwa mwili huo katika eneo la tukio bila kuhusisha polisi.

Bw Roy alifariki Februari 14, 2013, mjini Mombasa. Mzozo ulizuka ambapo wana hao wawili walishuku kuwa dada zao wa kambo Alexandra na Hellen na mama yao Din walihusika katika kifo hicho.

Hata hivyo, uchunguzi uliochukuwa miaka 10 ulihitimisha kuwa, hakuna ushahidi wa kutosha uliowasilishwa kuhusisha mtu yeyote na kifo cha tajiri huyo.

Wana hao wawili wamepinga matokeo ya uchunguzi huo katika Mahakama Kuu wakipinga jinsi mchakato wote wa uchunguzi ulivyoendeshwa katika mahakama ya hakimu.