Omondi na klabu yake ya Jonkopings waonja ushindi wa pili ligini Uswidi

Omondi na klabu yake ya Jonkopings waonja ushindi wa pili ligini Uswidi

Na GEOFFREY ANENE

JONKOPING Sodra anayochezea Mkenya Erick Johana Omondi ilizoa ushindi wake wa pili mfululizo kwenye Ligi ya Daraja ya Pili nchini Uswidi baada ya kuzima wenyeji GAIS kwa bao 1-0 mnamo Agosti 24 usiku.

Kiungo Robin Book alipachika goli safi dakika ya 84 mbele ya mashabiki 1, 664 ugani Gamla Ullevi mjini Goteborg. Book alimalizia gonga nipe gonga nikupe kutoka kwa Omondi na wachezaji wengine wawili akiwemo Edin Hamidovic aliyemmegea pasi ya mwisho.

Omondi alipata nafasi mbili nzuri murwa katika kipindi cha kwanza ikiwemo moja aliyofunga bao sekunde chache kabla kikatike, lakini akapatikana alikuwa ameotea.

Kiungo huyo mshambuliaji, ambaye kocha Jacob “Ghost” Mulee amemjumuisha katika kikosi chake cha Harambee Stars kwa mechi ya kufuzu kushiriki Kombe la Dunia 2022 dhidi ya Uganda (Septemba 2) na Rwanda (Septemba 5), alipumzishwa dakika ya 90.

Omondi anaongoza kufungia Jonkopings mabao. Yuko bega kwa bega na Adrian Edqvist baada ya kupachika mabao matano na kusuka pasi mbili zilizozalisha magoli.

Baada ya ushindi huo wa pili mfululizo, Jonkopings inashikilia nafasi ya saba kwa alama 27. Imejibwaga uwanjani mara 17 kwenye ligi hiyo ya klabu 16. Timu ya Vasalunds anayochezea kiungo mkabaji Anthony Wambani inapatikana katika mduara hatari wa kutemwa. Ilitoka 0-0 dhidi ya Helsingborg mnamo Agosti 23.

You can share this post!

Bournemouth wamtwaa mshambuliaji Morgan Rogers kutoka...

Ruto akataa talaka ya Uhuru