Habari

Omtatah afika kortini kupinga sheria mpya kwa madereva

March 20th, 2018 1 min read

Na RICHARD MUNGUTI

MWANAHARAKATI Okiya Omtatah amewasilisha kesi mahakamani kupinga kuzinduliwa kwa maagizo mapya kuhusu madereva.

Bw Omtatah anaomba Mahakama Kuu ibatilishe sheria za mtaala mpya uliotangazwa na Mamlaka ya Kitaifa ya Uchukuzi na Usalama (NTSA).

Mtetezi huyo wa wanyonge anasema kuwa sheria mpya za utoaji mafunzo kwa madereva na kuwahoji madereva wa magari ya uchukuzi wa umma upya yanakinzana na haki zao.

Bw Omtatah anasema masharti kwamba kila shule inayotoa mafunzo kwa madereva iwe na uwanja wa ekari 1.7  haifai.

NTSA inazitaka shule zote za kutoa mafunzo kwa madereva ziwe na uwanja mkubwa ndipo kuwe na barabara za kuwafundisha makurutu.

Pia zinatakiwa kuwa na majengo mazuri ya kutoa mafunzo. Omtatah anasema umma hakushirikishwa na NTSA kabla ya kupitisha sheria hizi.

NTSA ilitoa maagizo haya baada ya ajali kuongezeka haswa mwishoni mwa mwaka 2017.