Habari Mseto

Omtatah aokoa mabilioni ya walipa ushuru

March 14th, 2018 1 min read

Na RICHARD MUNGUTI

MAHAKAMA Kuu Jumanne ilimwokoa mlipa ushuru ilipofutilia mbali kandarasi ya Sh17 bilioni zilizokuwa zitozwe vinywaji visivyo vya kileo.

Mamlaka ya ushuru nchini KRA ilipata pigo kubwa ilipozimwa kuendelea na kandarasi iliyopewa na kampuni moja ya Uswizi ambayo ingekuwa inaweka stampu bidhaa zote zinazotengenezwa kwenye viwanda.

Baadhi ya bidhaa zilizokuwa zimelengwa ni pamoja na maji ya chupa na  vinywaji visivyo vileo.

Jaji John Mativo alifutilia mbali kandarasi iliyokuwa imepewa kampuni moja ya Uswisi ijulikanayo kama SICPA Securities Sol SA iliyokuwa imepewa kazi ya kuweka stampu bidhaa zote zinazotengenezwa kwenye viwanda.

Kampuni hiyo ya SICPA ilikuwa imepewa zabuni ya Sh4.8 bilioni na KRA kuiuzia serikali stampu maalum za kuweka katika bidhaa.

Mbali na stampu hizo, KRA ilikuwa imeipa kampuni hiyo ya Uswizi kandarasi ya kuwasilisha mitambo mingine ambayo ingetumika kutambua stampu bandia.

Akitoa agizo hilo, Jaji Mativo alisema arifa zilizochapishwa katika Gazeti rasmi la Serikali zilinakiliwa kwa njia inayokinzana na katiba na mwongozo maalum wa ulipaji kodi.

Jaji huyo alisema kandarasi iliyopewa kampuni hiyo ya Uswisi imepotoka na kwamba, maoni ya umma na washika dau hayakusakwa kabla ya kutolewa kwa kandarasi hiyo.

Bw Mativo alikubalia maombi la mwanahakarakati Bw Okiya Omtatah aliyeishtaki Serikali kwa sababu ya kandarasi hiyo akisema itawagharimu walipa ushuru mabilioni ya pesa.