Habari za Kitaifa

Omtatah arejea kortini kuripoti hofu kuhusu maisha yake

January 1st, 2024 2 min read

SAM KIPLAGAT na RICHARD MUNGUTI

SENETA wa Busia Okiya Omtatah amewasilisha kesi kortini kumshinikiza Inspekta Jenerali wa Polisi, Japhet Koome, awaagize maafisa wake kuandikisha taarifa yake kuhusu madai ya vitisho kwa maisha yake kwa kuwasilisha kesi ya kupinga Ushuru wa Nyumba.

Katika kesi aliyowasilisha Mahakama Kuu ya Nairobi, Bw Omtatah anasema anahofia vitisho alivyotoa Rais William Ruto mwezi uliopita wakati wa ibada ya kutoa shukran Kaunti ya Kisii.

Wakati wa ziara yake Kisii, Rais Ruto alisema: “Si mliona nilipewa upanga wakati nilipoapishwa? Nyinyi mnafikiri ulikuwa wa kukata mboga? Hapana… Ni wa kukabiliana na wakora wanaotupeleka kortini kuzuia miradi kama ya nyumba za bei nafuu.”

Bw Omtatah anasema matamshi ya Rais yalimlenga na kwa hivyo anahofia maisha yake yamo hatarini.

Seneta huyo anadai licha ya kuripoti suala hilo katika Kituo cha Polisi cha Lang’ata jijini Nairobi na Kituo cha Polisi cha Nyanchwa, Kisii, maafisa wa polisi wamekataa kuandikisha taarifa yake.

“Kwa hivyo mlalamishi amelazimika kuwasilisha ombi akiitaka korti, miongoni mwa mengine, kuwashurutisha washtakiwa (polisi) kuandikisha taarifa ya malalamishi yake kuhusu matusi na vitisho,” alisema kupitia nakala zilizowasilishwa kortini.

Anasema kuwa Dkt Ruto alitoa matamshi hayo mnamo Desemba 16, 2023 ambapo alimwita pamoja na walalamishi wengine wakora.

Seneta huyo wa Busia anasema suala hilo ni la dharura mno kwa sababu maafisa wa polisi wamekataa kumpa huduma za kitaifa anazostahili kupata, hususan fursa ya kuandikisha taarifa ya malalamishi ili uchunguzi uanzishwe.

“Mlalamishi ana hofia kuwa maisha yake binafsi na walalamishi wenzake yamo hatarini kabisa. Hivyo basi, anaomba hatua ya kisheria ichukuliwe kwa dharura ili kumpunguzia hofu na kumhakikishia usalama pamoja na wenzake,” alisema Bw Omtatah.

Anaeleza kuwa alijaribu kuwasilisha malalamishi mnamo Desemba 17 kuhusu alichotaja kama kudunisha mamlaka ya korti lakini hakupatiwa huduma hiyo.

Baada ya kukosa kuhudumiwa kwa muda wa zaidi ya saa sita, aliamua kwenda Kituo cha Polisi cha Mosocho kunakodaiwa kuwa ‘eneo la tukio’ lakini akazuiwa kuandikisha taarifa ya malalamishi katika Kituo cha Polisi cha Nyanchwa.

“Mlalamishi anahisi kuwa washtakiwa hawafai kuruhusiwa kukataa au kufeli kutekeleza wajibu wa umma waliotwikwa kisheria na hivyo kumhatarisha mlalamishi ambaye ana haki ya kutarajia wajibu huo utekelezwe,” anasema.

Anataka korti kuingilia kati upesi na kutoa amri ya kumshurutisha mkuu wa polisi na wadogo wake kutekeleza majukumu waliyotwikwa kikatiba kwa kurekodi taarifa yake ya malalamishi inavyohitajika kisheria.