Habari za Kitaifa

Omtatah awasilisha kesi kupinga Mswada wa Fedha wa 2024

May 22nd, 2024 1 min read

NA RICHARD MUNGUTI

SENETA Okiya Omtatah na mwanaharakati Eliud Karanja Matindi wamewasilisha kesi ya kupinga Mswada wa Fedha wa 2024 unaoashiria kuwatoza Wakenya kodi ya kufadhili bajeti ya Sh3.9 trilioni.

Mabw Omtatah na Matindi wanasema katika kesi iliyowasilishwa katika Mahakama Kuu kwamba mswada huo unakandamiza haki za Wakenya.

Wawili hao wameeleza kwa undani jinsi mswada huo unavyolenga kuwakandamiza Wakenya na kuvuruga haki zao ikiwa ni pamoja na kuongezewa kodi mbali mbali zitakapelekea bei ya bidhaa kama vile mikate kuongezeka.

Walalamishi hawa wanaomba mahakama kuu isitishe kabisa kujadiliwa kwa mswada huu na kuomba maoni ya umma.

“Endapo Bunge la Kitaifa litajadili mswada huu na kuuidhinisha kuwa sheria na kutiwa sahihi na Rais William Ruto itakuwa vigumu kuufutilia mbali,” inasema stakabadhi ya Bw Omtatah na Bw Matindi iliyowasilishwa kortini.

Ili kuwaepushia Wakenya kubebeshwa mzigo huu mzito wa kulipa kodi, Bw Omtatah na Bw Matindi wameomba mahakama ipige breki Bunge la Kitaifa kuujadili na kuzima hatua zozote za wananchi kuulizwa maoni yao kuhusu mswada huo.

Bw Omtatah ambaye ni nwanasiasa shupavu ameomba Jaji Mkuu Martha Koome ateue jopo la majaji wasiopungua watatu kusikiliza na kuamua kesi hiyo wanayosema iko na mashiko kisheria.

Mabw Omtatah na Matindi aidha wanaomba mahakama iharamishe Mswada wa Fedha wa 2024 uliochapishwa katika Gazeti Rasmi la Serikali Nambari 102 la 2024.

Katika kesi hiyo, Bw Omtatah amemshtaki Waziri wa Fedha Njuguna Ndung’u na Mwanasheria Mkuu.

Anaomba umma usikubaliwe kushirikishwa katika kupitishwa mswada huo anaosema unawakandamiza Wakenya wa tabaka mbalimbali.