Habari Mseto

Ondoa choo kichafu, Waziri Mutua aambiwa

February 2nd, 2024 2 min read

NA BRIAN OCHARO

WAZIRI wa Utalii na Wanyamapori Alfred Mutua atalazimika kuhamisha choo chake kilichoko katika makazi yake ya likizo huko Kilifi, ambayo kimekuwa kero kwa kutoa harufu mbaya kwa majirani kwa miaka mitano sasa.

Hii ni baada ya Mahakama ya Mazingira na Ardhi huko Malindi kukataa ombi la Waziri huyo kusitisha agizo la kumtaka kuhamisha choo hicho huku rufaa ambayo ananuia kuwasilisha ikisubirwa kusikilizwa na kuamuliwa.

Jaji Mwangi Njoroge aliamua kwamba mlalamishi katika kesi hiyo, Bi Fecilita Conte, ambaye amevumilia madhara hayo kwa miaka mitano, atapata madhara makubwa kuliko hasara atakayopata Waziri huyo iwapo choo hicho hakitahamishwa.

“Mshtakiwa (Dkt Mutua) anafaa kujiweka katika nafasi ya mlalamishi (Bi Conte) ambaye kilio chake cha kutaka haki kimethibitishwa kuwa cha kweli na mahakama hii. Pia, mshtakiwa anafaa kumhurumia mlalamishi kwa kutii amri ya mahakama hii katika suala hili ili amani iwepo kati ya majirani,” alisema jaji huyo.

Soma pia: Naomba unikome, Lilian aambia Mutua

Jaji alisema alizingatia ukweli kwamba matumizi ya mali ya mwanamke huyo yamepunguzwa sana kutokana na harufu ya choo hiyo na kwamba anaweza kupata madhara zaidi kuliko Dkt Mutua ikiwa hataruhusiwa kutekeleza uamuzi wa awali ya mahakama.

“Kwa upande mwingine, ni sehemu ndogo tu ya mali ya mshtakiwa itaathiriwa na utekelezwaji wa hukumu hiyo ambayo sidhani kama itakuwa hasara kubwa,” alisema jaji Njoroge.

Dkt Mutua aliwasilisha ombi hilo Agosti 9, ambapo aliiomba mahakama hiyo itoe agizo la muda kuzuia utekelezaji wa hukumu iliyotolewa Juni mwaka jana huku akisubiri kusikilizwa na kuamuliwa kwa rufaa aliyokusudia kuwasilisha.

Waziri huyo alilalama kuwa alipewa siku 45 pekee kuhamisha choo hicho ambacho ndicho kimezua mzozo na jirani yake.

Mwanamke huyo pia alikuwa amewasilisha ombi la kutaka Dkt Mutua afungwe kwa kukiuka amri ya mahakama au atozwe faini.

Kulingana na mwanamke huyo, Dkt Mutua aliwasilisha notisi ya kukata rufaa ya uamuzi wa mahakama badala ya kutii amri na maagizo ya kumtaka kuhamishaa choo hicho.

“Mshtakiwa pia ameshindwa kutii uamuzi wa mahakama, hivyo kunilazimu kuhama nyumba yangu na kukodisha sehemu nyingine hivyo kutumia gharama zisizostahili za Euro 3,561 (Sh626, 078),”alisema.

Hata hivyo, gavana huyo wa zamani wa Machakos alishikilia kuwa atakabiliwa na hasara iwapo ombi lake litakataliwa kwani mwanamke huyo anaweza kufanya ombi la kubomolewa kwa mali yake.

Soma pia: Mutua na Lilian wafunikia kiini cha kutengana

Mnamo Juni 8, mwaka jana, Jaji Millicent Odeny wa Mahakama ya Mazingira na Ardhi alimwagiza Waziri huyo kuhamisha choo hicho baada ya kukubaliana na Bi Conte kwamba chumba hicho kimekuwa kero kutokana na ukaribu wake na chumba chake cha kulia.

Jaji huyo alitoa uamuzi huo baada ya kubaini kuwa licha ya kupata vibali muhimu vya ujenzi, hatua hizi hazikutosha kutatua kero iliyosababishwa na kukamilika kwa choo hicho pamoja na tanki la maji taka.

Choo hicho kilicho kwenye chalet No.13 kinapakana na eneo la kulia la Bi Conte.