Ondoka Jack Grealish, ingia ?kiungo stadi Emi Buendia!

Ondoka Jack Grealish, ingia ?kiungo stadi Emi Buendia!

Na GEOFFREY ANENE

EMILIANO Buendia Stati ni mmoja wa wachezaji ambao Aston Villa inatumai kutumia msimu 2021-2022 kumaliza ukame wa miaka 40 bila taji la Ligi Kuu ya Uingereza.

Kiungo huyo mshambuliaji alijiunga na Villa tarehe mosi mwezi uliopita wa Julai.Alinunuliwa kwa Sh5.7 bilioni kutoka Norwich City.

Yeye ndiye mchezaji ghali katika historia ya Villa inayojivunia kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu mara 10. Kabla yake, winga Leon Bailey kutoka Jamaica alikuwa mchezaji ghali kambini mwa Villa baada ya kununuliwa kwa Sh4.5 bilioni kutoka Bayer Leverkusen.

Buendia, ambaye alipuuzilia mbali mavizio ya miamba wa Arsenal waliotaka huduma zake alipojiunga na Villa, alizaliwa mjini Mar del Plata nchini Argentina Sikukuu ya Krismasi mwaka 1996.

Alianza kukuza talanta yake ya soka katika klabu ya mtaani mwake ya Cadets de San Martin akiwa na umri wa miaka mitano.

Kisha, alielekea nchini Uhispania akiwa na umri wa miaka 11 kujiunga na akademia ya miamba Real Madrid.Hata hivyo, mwelekeo mzuri katika uchezaji wake ulipatikana kambini mwa akademia ya klabu ya Getafe alikofinyangwa kati ya Julai 1, 2010 na Julai 1, 2018 aliponyakuliwa na Norwich.

Kabla ya kuingia ligi ya Uingereza, Buendia alikuwa amepunguziwa dakika za uwanjani Getafe baada ya kupata jeraha la kifundo.

Baada ya kupona jeraha hilo mbaya, alipelekwa katika klabu ya daraja ya pili Cultural Leonesa kwa mkopo msimu 2017-2018.Kuhamishiwa kwake katika klabu hiyo maarufu kama La Cultu kulimsaidia sana katika kufufua soka yake.

Katika mechi 42 alizosakatia La Cultu, winga huyo alichana nyavu mara saba pamoja na kusuka pasi nane zilizozalisha magoli. Aliibuka mchezaji bora wa klabu hiyo.

Takwimu hizo zilishawishi Norwich kumvua Emi kutoka Getafe kwa Sh193.4 milioni (Yuro 1.5 milioni).

Norwich, ambayo ilikuwa ikishiriki Ligi ya Daraja ya Pili, ilimsaini kwa kandarasi ya miaka minne. Bao lake la kwanza kabisa akiwa Norwich ni dhidi ya Brentford katika ushindi wa 1-0 mnamo Oktoba 2018.

Alijitokeza kuwa tegemeo katika ubunifu msimu huo wa 2018-2019. Alichangia jumla ya mabao manane na kumega pasi 12 zilizozaa matunda klabu hiyo ikipandishwa ngazi kushiriki Ligi Kuu ya msimu 2019-2020.

Kwa jumla, Buendia alisakata michuano 121 akiwa ugani Carrow Road akichangia magoli 24 na pasi 42 zilizofungwa katika misimu yake mitatu.

Nguvu zake ni katika kuundia wenzake nafasi za kufunga mabao. Itakumbukwa kuwa Desemba 2019 aliunda nafasi 29.

Idadi hiyo ni kubwa kuwahi kushuhudiwa kutoka kwa mchezaji mmoja katika kipindi cha mwezi mmja tangu takwimu hizo zianze kunakiliwa msimu 2003-2004.

Bao lake la kwanza la Norwich kwenye Ligi Kuu lilipatikana katika kichapo cha 2-1 mikononi mwa Watford mnamo Julai 7 mwaka jana.

Norwich ilitemwa msimu huo wa 2019-2020.Msimu uliopita, Buendia alipachika mabao 15 na kuchanja pasi 17 zilizokamilishwa kuwa magoli.

Ufanisi huo uwanjani ulishuhudia akitawazwa mchezaji bora wa msimu wa Ligi ya Daraja ya Pili pamoja na mchezaji bora wa Norwich iliyoshinda ligi hiyo na kupandishwa ngazi kushiriki Ligi Kuu msimu 2021-2022.

Villa inatumai atakuwa kizibo tosha cha Jack Grealish ambaye ameyoyomea Manchester City.Kimataifa, Buendia amewahi kuchezea timu ya Uhispania pia Argentina.

Alikuwa katika kikosi cha Uhispania cha wachezaji wasiozidi umri wa miaka 19 ikipimana nguvu dhidi ya Ujerumani na Ugiriki na kutiwa kitini dhidi ya Ufaransa mnamo Novemba 2014.

Argentina ilimnyakua na kumtumia katika mechi nne za kimataifa za wachezaji wasiozidi umri wa miaka 20 mwaka 2015 zikiwemo tatu katika Kombe la Dunia nchini New Zealand.

Emi hatajapata kuchezea Argentina tena, ingawa alijumuishwa katika kikosi cha watu wazima cha Argentina mwezi Mei 2021 kwa dimba la Copa America bila ya kufaulu kuingia kikosi cha mwisho.

Mchezaji huyu, ambaye ana ndugu wawili, ameoa raia mwenzake kutoka Argentina, Claudia na wamejaliwa na mtoto wa kiume, Thiago. Ripoti nchini Uingereza zinasema atakuwa akipokea mshahara wa Sh11.3 milioni kila wiki ugani Villa Park.

You can share this post!

Bondia Okwiri apiga dafrau Fidel Munoz wa Colombia

Yaibuka Wizara ya Utalii imemumunya mabilioni ya pesa za...