Makala

ONGAJI: Ajali barabarani zitaepukika kwa kuwa waangalifu tu

July 13th, 2020 2 min read

Na PAULINE ONGAJI

NI siku chache zimepita tangu Rais Uhuru Kenyatta aondoe marufuku ya usafiri kutoka kaunti moja hadi nyingine; amri ambayo alikuwa ameitoa ili kukabiliana na maambukizi ya virusi vya corona.

Lakini hata kabla ya kupumua, familia za Wakenya tisa zinaomboleza vifo vya jamaa zao waliofariki katika ajali mbili tofauti, moja eneo la Kitui, na nyingine katika sehemu ya Eldoret.

Mbali na kusababisha vifo, ajali hizi mbili pia ziliwaacha wengine na majeraha mabaya.

Hii ni asilimia ndogo tu ya visa vya ajali za kusikitisha kwenye barabara zetu; kumbukumbu ya jinamizi ambalo limetawala sekta ya usafiri wa umma nchini, kwa miaka mingi.

Kulingana na takwimu zilizotolewa na Halmashauri ya Kitaifa ya usafiri na Usalama (NTSA) Desemba mwaka jana, watu 3,409 walifariki kutokana na ajali za barabarani wakati huo.

Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO) kati ya Wakenya 3000 na 13 000 hupoteza maisha yao kupitia ajali za barabarani kila mwaka.

Takwimu hizi zinaashiria utovu wa nidhamu katika sekta hii huku raia wakiendelea kuumia, na familia zikiomboleza vifo vya wapendwa wao waliopoteza maisha yao ghafla.

Kwa upande mwingine, wahalifu wanaokiuka sheria za barabarani wanaendelea kufurahia uhuru wao na kuhudumu katika barabara zetu.

Kumekuwa na video za magari ya usafiri ya umma yakiendeshwa kiholela barabarani lakini hakuna hatua inayochukuliwa kukabiliana na utovu huu wa sheria.

Kinachosikitisha ni kwamba, mara nyingi magari husika yanaposababisha vifo, hupokonywa leseni za kuhudumu kwa muda mfupi, kisha kurejea barabarani kisiri au magari hayo kubadilisha majina na kuendelea na kazi.

Na kinachohuzunisha ni kwamba, waathiriwa wengi wa janga hili hawapati haki.

Aidha, licha ya magari hayo kujiunga na vikundi mbalimbali vya ushirika yaani Sacco, hakujaonekana matunda yoyote hasa katika masuala ya nidhamu miongoni mwa wahudumu wa magari ya usafiri wa umma.

Ukweli ni kwamba, suala la nidhamu na uzingatiaji sheria katika magari ya usafiri wa umma na barabara za Kenya kwa jumla limekuwa donda sugu.

Wakati umewadia kwa zimwi hili kukabiliwa hadharani, la sivyo Wakenya waendelee kufa barabarani.

Hasa msimu huu ambapo kutokana na amri ya kupunguza idadi ya abiria kwenye magari ya umma inapoendelea kutekelezwa, vile vile kafyu, inamaanisha madereva wengi wataendelea kukiuka sheria za trafiki katika harakati ya kulipisha upungufu wa mapato kutokana na masharti haya.