Makala

ONGAJI: Karaha kwenye barabara kuu ya Thika zitatuliwe

April 15th, 2019 2 min read

Na PAULINE ONGAJI

TANGU ilipozinduliwa miaka saba iliyopita, barabara kuu ya Thika imesaidia kupunguza msongamano wa magari na hivyo kurahisisha usafiri. Kwa upande mwingine, pia imekuza baadhi ya madereva na manamba wakorofi zaidi nchini.

Ni nadra kwa mwezi kupita bila kisa cha utovu wa nidhamu kinachohusisha magari ya usafiri wa umma kuripotiwa kwenye barabara hiyo ambapo baadhi huwa vya kutisha vinavyosababisha maafa ya wananchi.

Hivi majuzi, kwa mara nyingine, maisha ya Mkenya yalikatizwa kutokana na kutojali kwa dereva katika baraba hii.

Nazungumzia kisa cha mwanamke aliyeachwa kilema baada ya basi la kampuni ya Neo Kenya Mpya kumgonga bila huruma likiendeshwa kiholela.

Ingawa kampuni hiyo inasemekana kuahidi kushughulikia gharama za matibabu za mwanamke huyo, bado inahitajika hatua zichukuliwe kurudisha nidhamu katika barabara kuu ya Thika.

Wahudumu wa basi la kuelekea mtaani Githurai waliwahi kuhukumiwa kifo baada ya kupatikana na hatia ya kumdhulumu kimapenzi na kumpora binti fulani kwenye gari.

Vivyo hivyo, wahudumu wa matatu walisemekana kusababisha kifo cha kipusa mmoja wa chuo kikuu baada ya kumsukuma kutoka kwa basi lililokuwa likienda katika barabara hii.

Majuma machache yaliyopita, video ilisambazwa mitandaoni ikionyesha wahudumu wa matatu Lopha wakimchapa abiria kiasi cha kuvuja damu.

Hii ni mifano michache ya utovu wa nidhamu miongoni mwa wahudumu wa magari ya usafiri wa umma yanayotumia barabara hiyo.

Miaka mitatu iliyopita, takwimu za Mamlaka ya Kitaifa ya Uchukuzi na Usalama (NTSA) zilionyesha barabara hiyo ilikuwa hatari zaidi jijini Nairobi.

Iliwakilisha asilimia 30 ya vifo vilivyotokana na ajali jijini Nairobi huku ulevi na utovu wa nidhamu miongoni mwa madereva ukichangia pakubwa.

Lakini hauhitaji kuwa mtaalamu wa uchukuzi kuelewa kwamba, wahudumu hawa wanazidi kuwa hatari kwa usalama wa abiria na wapita njia.

Ili kupata picha kamili ya kiwango cha wendawazimu miongoni mwa baadhi ya wahudumu wa magari ya kutumia barabara hii, tembelea kituo cha mabasi cha Nyamakima.

Kituo hiki huegeshwa magari ya kuelekea baadhi ya mitaa kwenye barabara kuu ya Thika, miongoni mwao Githurai, Zimmerman na Kahawa.

Unapotembelea eneo hili, hasa giza linapobisha, ni rahisi kudhani uko katika taifa lisilotawaliwa na sheria. Katika harakati za kubeba abiria, mabasi haya huwa yameegeshwa katikati mwa barabara kiasi kwamba, hakuna magari mengine yanaweza kupita, na hivyo kusababisha msongomano mkubwa wa magari wakati wa jioni.

Cha kushangaza ni kwamba, watumizi wengine wa barabara hawana budi ila kutii, la sivyo wajipate katika hatari ya kushambuliwa na wahudumu hawa.

Mara nyingi, uovu huu huendelea machoni mwa polisi wa trafiki. Iwapo waziri wa Uchukuzi atataka kukabiliana na utovu wa nidhamu miongoni mwa wahudumu wa matatu nchini, basi mtihani mkubwa uko kwenye barabara kuu ya Thika.

Iwapo haya hayatabadilika, vifo na majeraha kwenye barabara hii vitaendelea kusalia takwimu tu!