Makala

ONGAJI: Kenya Power ina wajibu wa kulinda maisha ya Wakenya

August 24th, 2020 2 min read

Na PAULINE ONGAJI

KWA siku kadhaa sasa sehemu ya mtandao wa kijamii imetawaliwa na picha moja ya kuhuzunisha.

Picha hiyo inamuonyesha mwanamke aliyefariki kichakani baada ya kuuawa kwa umeme katika kijiji cha Bowa ya Matopeni, Kaunti ya Kwale.

Kinachohuzunisha hata zaidi ni kwamba mama huyo alikutana na mauti akiwa amembeba mwanawe machanga mgongoni, ambapo pia yeye hakusazwa kutokana na makali ya umeme.

Hiki sio kisa cha kwanza kwani tatizo la watu kuuawa kwa umeme limekuwepo ambapo mara nyingi shirika la usambazaji umeme la Kenya Power limekuwa likielekezewa kidole cha lawama na kushtumiwa kwa utepetevu.

Lakini kwa upande wake, shirika la Kenya Power limejitokeza mara kwa mara kujiondolea lawama kutokana na visa hivi.

Miaka mitatu iliyopita shirika hili lilizindua ripoti iliyoonyesha kwamba janga la binadamu kuuawa kwa umeme nchini ni donda sugu huku angaa vifo vya watu sita vikiripotiwa kila mwezi.

Aidha, ripoti hiyo ilionyesha kwamba asilimia 32 ya visa hivi vinatokana na ajali nyumbani kutokana na mfumo mbovu wa nyaya za umeme, vile vile uunganishaji haramu wa umeme.

Aidha, shirika hili limekuwa likilaumu wizi wa nyaya za umeme na uingiliaji wa ardhi ambamo nyaya za umeme zimeunganishwa kama baadhi ya sababu ambazo zimechangia kuendelea kuongezeka kwa visa hivi.

Ni suala ambalo bila shaka halipingwi lakini lazima ieleweke kwamba asilimia kubwa ya visa hivi pia ni kutokana na nyaya zenye umeme mtaani ambazo zimeendelea kuhatarisha maisha ya wengi.

Kumekuwa na visa vya watoto watoto wanaouawa kwa umeme wanapokanyaga nyaya hizi wakicheza. Kumekuwa na visa vya watu wazima kuuawa na kujeruhiwa vibaya na nyaya hizi.

Hata kumekuwa na visa vya wafanyakazi wa shirika hili kunusurika wakiwa katika harakati za kurekebisha nyaya za umeme.

Visa hivi ni ishara tosha kwamba wakati umewadia kwa tatizo hili kuchukuliwa kwa umakini unaostahili. Lakini kinachoshangaza ni kwamba mara kwa mara kunapotokea visa vya aina hii, badala ya suluhu ya kudumu kuwepo, watu wameendelea kulaumiana.

Naam, bila shaka Wakenya wamechangia pakubwa katika ajali zinazotokana na nguvu za umeme, lakini shirika hili kama taasisi iliyo na mamlaka ya kusambaza umeme nchini, ina nguvu na rasilimali za kupambana na janga hili, ikilinganishwa na raia wa kawaida ambaye katika shughuli zake za kawaida, kwa bahati mbaya alikumbana ana kwa ana na nyaya hizi.