Makala

ONGAJI: Mashirika yameanika udhaifu wa sekta ya afya Afrika

September 17th, 2020 2 min read

Na PAULINE ONGAJI

Hivi majuzi kuliibuka mtafaruku baina ya mashirika mawili yasiyo ya kiserikali nchini, kuhusu udhibiti wa fedha zilizokuwa zimetolewa kwa minajili ya matibabu ya maradhi kadhaa nchini.

Uhasama huo ulikuwa kuhusu pesa za msaada zilizokuwa zimetolewa na shirika la Global Fund katika vita dhidi ya maradhi ya Ukimwi, malaria na kifua kikuu.

Ni suala lililosababisha shirika hilo kusitisha matumizi ya kitita hicho cha zaidi ya Sh12 bilioni, huku hazina hiyo ikilalamikia shughuli ya uteuzi wa shirika ambalo mwanzoni lilikuwa limepewa mamlaka ya udhibiti wa fedha hizo.

Tukio hili linaonyesha jinsi pesa za msaada hasa katika sekta ya afya sio tu nchini bali barani, zina thamani sana kiwango cha kusababisha uhasama mkali baina ya mashirika ambayo lengo lao kuu ni kushughulikia waathiriwa wa maradhi husika.

Kinachohuzunisha zaidi ni kwamba hili ni donda sugu katika sekta za matibabu katika mataifa mengi barani zinazoendeshwa na mashirika yasiyo ya kiserikali, tofauti na nchi zingine ambapo hili ni jukumu la serikali.

Kumbuka kwamba mashirika haya hasa hutegemea ufadhili na misaada kutoka ng’ambo, ambapo swali kuu ni je serikali kwa upande wake ina mfumo au uwezo wa kukagua matumizi ya fedha hizi?

Kunao wanaoohoji kwamba suluhisho ni kwa mataifa ya Afrika kuwekeza zaidi katika sekta za afya na matibabu, lakini hii itawezekanaje ikiwa mataifa ya Afrika hayako tayari kudhibiti sekta hii?

Kwa mfano, mwaka wa 2001, kupitia Azimio la Abuja (Abuja Declaration), nchi nyingi ziliahidi kutumia angaa asilimia 15 ya bajeti ya mwaka katika masuala ya kiafya, ilhali ni chache ambazo zilitimiza lengo hili.

Mwaka wa 2018, Andreas Seiter, kiongozi wa sekta ya kibinafsi katika masuala ya afya, lishe na idadi ya watu kwenye Benki ya Dunia alisema kwamba, kwa kawaida mataifa ya Afrika hayatengei sekta ya afya pesa za kutosha.

Aidha, kulingana na Seiter, hata ufadhili huu unapotolewa, mataifa mengi ya Afrika yamekuwa na tabia ya kuelekeza fedha zilizokuwa zimetengewa matumizi ya afya, katika sekta zingine.

Hii inamaanisha kwamba asilimia kubwa ya bajeti ya afya katika mataifa haya inaachiwa ufadhili wa kutoka nje. Ni suala linaloachia mashirika yasiyo ya kiserikali mwanya wa kudhibiti sekta hii, na hivyo kuhatarisha afya ya wagonjwa tukio la aina hii linapoibuka.