Makala

ONGAJI: Ukosefu wa kazi umeumbua na kudhalilisha vijana wetu

July 19th, 2020 2 min read

Na PAULINE ONGAJI

HIVI majuzi, niliamshwa na vurumai karibu na nyumbani kwangu. Nilipotoka nje, nilikumbana na kundi la vijana waliokuwa wamejazana pomoni katika matatu, huku wengine wakining’inia kwenye paa la gari hilo.

Baadhi ya vijana walining’inia kwenye magari mengine yaliyokuwa nyuma ya matatu hiyo, wengine walikuwa kwenye pikipiki, na baadhi wakitembea.

Kilichovutia macho ya wengi ni kelele za vijana hawa waliokuwa wakipiga pamoja na mbinja, huku wengine wakionekana kana kwamba walikuwa wamebugia vileo au mihadarati fulani.

Nilipohoji kilichokuwa kikijiri, nilifahamishwa kwamba, walikuwa katika harakati za kukaribisha gari hilo jipya barabarani, ambapo hiyo huwa ada kabla ya matatu kuanza rasmi shughuli za uchukuzi.

Kwa kawaida, wenye matatu hutumia vijana wa aina hii ‘kutambulisha’ magari mapya kwa wateja, na kwa upande wao wanapokea malipo madogo kutokana na huduma zao.

Japo kuna baadhi ya watu wanaohisi hii ni mbinu ya kuwapa vijana kipato, matukio ya aina hii yanaakisi uhaba wa ajira miongoni mwa vijana wetu, na ni dhihirisho la jinsi wanavyotumiwa vibaya.

Ikiwa sio kuzindua bidhaa fulani, ni kufanyia wanasiasa kampeni ambapo hapa ni wao wanaostahimili na kuvumilia jua kali, na hata wakati mwingine kubugia vitoa machozi, tatizo linapotokea.

Kukiwa na migogoro baina ya wanasiasa, ni wao wanaotumiwa kuwakabili wapinzani, na katika harakati hizo kujeruhiwa au hata kupoteza maisha yao.Aidha, kuna mashirika mengi ambayo pia yamekuwa yakiwatumia vijana kueneza jumbe za uwongo kuhusu jinsi ya kutajirika upesi kwa kutumia bidhaa au huduma zao.

Pia, pengine umekutana na makundi ya vijana mijini wanaotumiwa na wafanyabiashara laghai, ambapo kazi yao ni kunasa raia wasiojua na kuwadanganya waingie kwenye mashindano ya uwongo ili wajishindie bidhaa mbali mbali.

Katika shughuli hizi zote, vijana hunaswa na zawadi ndogo ndogo kama vile tishati au senti kidogo.Kuna wale wanaowalaumu vijana kwa kukubali kunaswa na zawadi hizo ndogo ndogo, lakini ukweli ni hata tunapowanyoshea kidole cha lawama pia tunapaswa kutilia maanani kwamba, wengi wao wanafanya hivyo angaa kupata riziki.

Vijana hawana kazi na wanahangaika huku nje, suala linalodhihirika na jinsi wako tayari kushawishika na senti kidogo ili kufanya kazi zinazoonekana kuwashusha hadhi na kuwapunguzia heshima.

Sawa na jinsi mzazi anayewajibika anavyomtunza mwanawe, serikali inapaswa kuwalinda vijana, na hakuna njia mwafaka ya kufanya hivyo ikiwa sio kuwepo kwa mfumo unaowapokea na kuwawezesha vijana kujitegemea, pindi wanapokamilisha masomo.