Makala

ONGAJI: Viongozi wa Afrika ndio kiini kikuu cha umaskini barani

July 27th, 2020 1 min read

Na PAULINE ONGAJI

NCHINI Msumbiji kuna mradi wa kuinasua jamii moja inayoishi kando ya mbuga ya wanyamapori kutokana na umaskini.

Wakazi hawa wanakumbwa na hali ngumu ya maisha ikiwemo uhaba wa chakula na huduma za afya.

Hili ni jambo la kusikitisha ikizingatiwa kwamba Msumbiji ni mojawapo wa mataifa yaliyo na utajiri mkubwa wa rasilimali asili barani Afrika hasa gesi asili, suala ambalo limevutia baadhi ya mashirika makubwa ya kimataifa ya uzalishaji nishati nchini humo.

Lakini licha ya uwekezaji huo wa thamani ya mabilioni ya pesa, raia wa nchi hiyo wanaendelea kukumbwa na umaskini wa viwango vya juu.

Hili sio tatizo linaloikumba nchi hii pekee barani Afrika, kwani licha ya mataifa kuwa na rasilimali nyingi, raia wanaendelea kuangamia katika ufukara.

Kwa mfano, Nigeria inaorodheshwa miongoni mwa mataifa yanayozalisha mafuta kwa wingi ulimwenguni, lakini kinaya ni kuwa taifa lilo hilo ni kati ya mataifa yenye miundomsingi duni zaidi duniani.

Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) nayo ina utajiri mkubwa wa dhahabu, almasi, kobalti, shaba nyekundu na bati, miongoni mwa madini mengine, lakini ni mojawapo ya mataifa yanayotawaliwa na ghasia na umaskini mkubwa duniani.

Hapa Kenya, licha ya taifa hili kuorodheshwa nambari moja barani Afrika, na namba nne ulimwenguni kwa uzalishaji majani chai, wakulima hawana mengi ya kujivunia kutokana na kilimo cha zao hili.

Isitoshe, huku Kenya ikiendelea kuongoza kwa usalishaji wa kiwango kikubwa cha majanichai na mazao mengine, taifa hili liko miongoni mwa nchi zinazoshikilia mkia katika suala la utoshelezi wa chakula.

Taarifa hizi zote zinaashiria jinsi Afrika licha ya kubarikiwa vilivyo kwa rasilimali, bado inaendelea kusalia nyuma kimaendeleo.

Kuna wale wanaohoji kwamba mataifa ya Afrika yamekuwa yakikandamizwa na mataifa ya Magharibi, kwa minajili ya kufyonza rasilimali zao.

Lakini ukweli wa mambo ni kuwa viongozi wa Afrika ndio wanafanikisha uporaji huu wa raslimali za mataifa yao na kuwaacha wenyeji wakiteseka.