Makala

ONGAJI: Wakati wa vyombo vya habari vya Kiswahili kuzinduka ni sasa

May 13th, 2019 2 min read

Na PAULINE ONGAJI

NINA uhakika kwamba umepata fursa ya kukutana na picha za kejeli mtandaoni almaarufu kama ‘meme’ wakati wowote unapopekua mitandao ya kijamii.

Majuma kadha yaliyopita, nilikutana na meme moja kwenye mtandao wa kijamii ambapo kulikuwepo picha ikilinganisha habari zinazopewa kipaumbele na vyombo vya habari humu nchini na zile ambazo huwa zinapeperushwa na stesheni nyingine za kimataifa.

Picha mbili za kwanza zilikuwa zinaonyesha vituo fulani vya kimataifa ambapo mada ilikuwa kuhusiana na ustawi wa vijana na masuala ya kiteknolojia.

Kwa upande mwingine, picha ya tatu ilikuwa ya habari za lugha ya Kiswahili za stesheni moja hapa nchini, ambapo mada ilikuwa iwapo mabinti wanapaswa kuvalia chupi au la.

Hii ni meme iliyoibua hisia kali mtandaoni huku maoni mengi yakiwa kuhusu ni habari zipi zinazopewa umuhimu na vyombo vya habari vya humu nchini, hasa vinavyopeperusha matangazo yao kwa lugha ya Kiswahili kwenye redio na runinga.

Maoni mengi yalionekana kukemea baadhi ya vitengo vinavyopeperusha matangazo yao kwa lugha ya Kiswahili kwa kutawaliwa na mada za mzaha na zisizo na kina.

Wengi walitaja hizo kama baadhi ya sababu zinazowafanya wasitazame taarifa za habari kwa lugha ya Kiswahili, na badala yake kusubiri zile zinazopeperushwa kwa Kiingereza ili kupata kina cha matukio yanayoendelea nchini na kimataifa.

Ilikuwa ni hoja ambayo nakubaliana nayo kwa asilimia fulani. Majukwaa mengi ya habari za Kiswahili yameshushwa thamani na kuwa ya kuzungumzia masuala ya kipumbavu wakati mwingi kuliko muda unaotolewa kujadili masuala yaliyo na umuhimu katika jamii. Hii inafanyika huku yakitarajiwa kushindania hadhara na mengine yanayopeperusha matangazo kwa lugha ya Kiingereza ambayo mara nyingi huzungumzia masuala ya kina na yenye umuhimu mkubwa kwa jamii kama vile ustawi wa kiuchumi, teknolojia na sayansi.

Ni kana kwamba hadhara ya wanaotazama au kusoma taarifa kwa lugha ya Kiswahili ni watu wasio na elimu au wasioelewa mambo yanavyoendelea ulimwenguni.

Ni kwa sababu ya haya ambapo lugha hii imezidi kudharauliwa kiasi cha kwamba imekuwa kawaida kwa watu wakomavu waliopitia mfumo wa elimu humu nchini unaohusisha masomo ya Kiswahili, kusema bila aibu kwamba hawawezi kuzungumza lugha hii.

Inahuzunisha sana hasa ikizingatiwa kuwa Kiswahili kimevuka mipaka kiasi cha kuwa sasa kinazungumzwa katika mataifa mengi barani, huku Afrika Kusini ikitangaza hivi majuzi kwamba kinapangiwa kuhusishwa katika mtaala wa masomo nchini humo.

Wakati umefika kwa vyombo hivi vya habari kuipa lugha hii heshima inayostahili na kuwekeza kuhakikisha kwamba utaalamu unaotumika kupeperusha taarifa kwa lugha ya Kiingereza, pia unazingatiwa katika vitengo vya Kiswahili.

Ikiwa tunataka kukuza na kuipa lugha ya Kiswahili heshima inayostahili sharti basi tupanue hadhara, jambo litakaloafikiwa kwa kuhakikisha kuwa habari zinazopeperushwa kwa lugha hii zinavutia watu kutoka ngazi mbali mbali kijamii, kimasomo, kitaaluma na hata kiuchumi.

[email protected]