Makala

ONGAJI: Wakenya wasifumbie shida zao wakianika wengine mitandaoni

June 29th, 2020 2 min read

Na PAULINE ONGAJI

WAKENYA wanafahamika ulimwenguni kote kwa mambo mengi.

Vita vinapochipuka kwenye mtandao wa Twitter, ni wachache ulimwenguni wanaweza kukiri kuwafikia Wakenya kwa kiwango cha ubishani kwenye jukwaa hili.

Ni suala ambalo hivi majuzi lilidhihirika Wakenya walipoungana na watu kutoka sehemu zingine ulimwenguni kupinga ubaguzi wa rangi nchini Amerika, donda ambalo kwa miaka limekumba mifumo katika taifa hilo.

Ujuaji wa Wakenya ulijitokeza hata zaidi kwani bendera ya Kenya ilionekana mara kadha katika baadhi ya maandamano nchini humo, na hata Mkenya kuwafunza Waamerika kauli mbiu maarufu ya ‘haki yetu’.

Kinachoshangaza ni kwamba hapa, Wakenya walijifanya kuwa wataalamu wa kupinga ubaguzi wa rangi, huku wakifumbia macho uhalisi wa ubaguzi wa kikabila hapa nchini.

Kwa mfano, sawa na ubaguzi wa rangi unaoendelea dhidi ya watu weusi nchini Amerika, pia hapa Kenya kuna sehemu ambazo wewe Mkenya huwezi kufanya shughuli zozote, kumiliki kipande cha ardhi au kuendesha biashara ikiwa wewe si mwenyeji.

Nazungumzia nchi ambayo mtu anaweza kumtusi mwenziwe hadharani eti kwa sababu yeye ni wa kabila tofauti, huku ukabila ukiwa mojawapo ya vigezo vinavyotumika kugawa nafasi za kazi na fursa zingine.

Kenya ni nchi ambayo kiongozi anachaguliwa na kugawanya raia kwa msingi wa kikabila hadharani, huku akiamua sehemu zipi zitakazonufaika na rasilimali za kitaifa.

Hii ni nchi ambayo mwanamuziki anaweza kutunga wimbo kwa lugha ya mama na kuwatusi watu kutoka sehemu fulani, na hata nyimbo zake zichezwe katika maeneo ya umma pasi na wasiwasi wa kuchukuliwa hatua za kisheria.

Itakuaje kwamba tunachukiana licha ya kuwa na rangi sawa ya ngozi, ilhali tunatarajia kuwashurutisha watu wa asili tofauti kutukubali?

Kumbuka kwamba ni mfumo huu unaotumika kuwakandamiza Waafrika nchini Amerika, ndio huo huo unaotumika kueneza itikadi za kikabila hapa Kenya.

Sawa na ubaguzi wa rangi, ukabila pia umekuzwa kupitia fikra ambapo kuna baadhi ya watu wanaojiona kuwa na hadhi zaidi ya wengine, na hivyo wanastahili kunufaika na rasilimali za kitaifa zaidi ya wengine.

Kwa ufupi, baadhi ya Wakenya wanapaswa kufyata midomo hasa kuhusu ubaguzi wa rangi nchini Amerika, kwani wao ni watekelezaji wakuu wa ubaguzi wa kikabila hapa nchini.

Na ukiniuliza, ukabila ni uovu zaidi ukilinganishwa na ubaguzi wa rangi, kwani wewe Mwafrika unamkandamiza na kumdhulumu mwenzio anayefanana nawe, katika ulimwengu ambapo mtu mweusi anakumbana na chuki kutoka kwa watu wa asili zingine.