Habari

Ongeri achaguliwa mwenyekiti wa CPAIC

June 25th, 2020 1 min read

Na CHARLES WASONGA

HATIMAYE Seneta wa Kisii Sam Ongeri amechaguliwa kuwa mwenyekiti wa Kamati ya Uhasibu wa Pesa za Umma katika Kaunti (CPAIC) baada ya mwenzake wa Narok Ledama Ole Kina kujiondoa.

Bw Ledama alichukua hatua hiyo Mei 2020 kutokana na shinikizo kutoka chama cha ODM ambacho kilimpendekeza Prof Ongeri kwa wadhifa huo.

Hii ni baada ya Seneta huyo wa Narok kuibuka mshindi katika uchaguzi uliofanyika Mei 4, 2020, kwa kupata kura tano huku Ongeri akipata kura nne.

Lakini baada ya ODM kutisha kumwadhibu Ledama kwa kumfurusha kutoka kamati hiyo na ile ya kuratibu shughuli za Seneti (SBC), aliamua kuachia wadhifa huo.

Ndiposa Ledama alikubali kujiondoa kutoka uenyekiti wa CPAIC baada ya kukutana na kiongozi wa ODM Raila Odinga na “kuomba msamaha”.

Katika uchaguzi wa Alhamisi, Prof Ongeri amechaguliwa bila kupingwa huku Seneta wa Marsabit Harugura Godana akichaguliwa kuwa naibu wake.

Sasa Bw Ledama atasalia kuwa mwanachama wa kawaida wa CPAIC ambayo huchunguza madai ya wizi na matumizi mabaya ya pesa za umma katika serikali zote 47 za kaunti.

Wanachama wengine wa kamati hiyo ni; Fatuma Dullo (Isiolo), Johannes Mwaruma (Taita Taveta), Charles Kibiru (Kirinyaga), Kimani Wamatangi (Kiambu) na Irungu Kang’ata (Murang’a).