Habari Mseto

Ongezeko la wahuni wa ‘Marachi Boys’ kwenye mikutano ya kisiasa lazua hofu

April 13th, 2024 2 min read

NA JESSE CHENGE

KAMISHNA wa Kaunti ya Bungoma, Thomas Sankei, ametoa tahadhari kuhusu ongezeko la wahuni wanaoshiriki maandamano pamoja na mikutano ya kisiasa ya wanasiasa katika hafla za umma.

Hali hii anasema inatishia usalama wa wanahabari na wananchi kwa ujumla, akieleza haya katika warsha ya Usalama iliyoandaliwa na Baraza la Vyombo vya Habari Kenya (MCK) mjini Bungoma.

Kamishna Sankei amesisitiza umuhimu wa kuimarisha usalama na amewataka wanasiasa kuacha kuhatarisha maisha ya wananchi kwa kushirikiana na wahuni hao.

“Mazingira ya sasa yanahitaji kuwa na usalama imara, na pia wanasiasa wanapaswa kuelewa kuwa kuhatarisha maisha ya wananchi ni jambo lisilokubalika,” alisema Kamishna Sankei.

Amewahimiza wanahabari kuwa makini na taarifa zinazozua uhasama miongoni mwa viongozi. Ametoa mfano wa kauli za kisiasa zilizosababisha utata kati ya Spika wa Bunge la Kitaifa, Moses Wetang’ula, na Gavana wa Trans-Nzoia, George Natembeya.

“Ni muhimu kwa wanahabari kuzingatia umakini na kuepuka kuchapisha taarifa ambazo zinaweza kuchochea uhasama na kuhatarisha amani,” aliongeza Kamishna Sankei.

Ongezeko la wahuni wanaoshiriki mikutano ya wanasiasa katika hafla za umma katika Kaunti ya Bungoma limekuwa tishio la usalama kwa wanahabari na hata kwa wananchi wote.

Waziri wa Usalama Kithure Kindiki alipozuru magharibi majuzi alitoa taarifa kuhusu wasiwasi uliopo kuhusu vijana wa ‘Marachi Boys’ wanaodaiwa kuhangaisha wakazi huko Busia.

Vijana hao wamekuwa wakiwatisha watu katika eneo hilo. Kindiki ameitaka idara ya usalama katika eneo hilo kuchukua hatua za dharura dhidi ya makundi hayo ya wahalifu, ambao pia wanaeneza uhalifu wao katika kaunti za Bungoma na Vihiga.

“Wasiwasi umekuwepo kuhusu vijana wa Marachi huko Busia ambao wamekuwa wakiwatisha watu katika eneo hilo,” alisema Kindiki.

Aidha, Kindiki ametoa onyo kwa magenge ya majambazi katika eneo la Magharibi, ikiwemo ‘Jobless group au Marachi Boys gang’ kwamba hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yao. Amewataka magenge hayo kuacha tabia zao za uhalifu mara moja.

“Magenge ya majambazi eneo hili la Magharibi chuma chao ki motoni na watakumbana na mkono mkali wa sheria,” Kindiki alisema.

Aliyasema haya wakati wa uzinduzi wa afisi ya Naibu Kamishna eneo la Musanda Mumias Magharibi.