Habari Mseto

Ongoro, mumewe wamulikwa

October 25th, 2019 1 min read

Na MARY WANGARI

ALIYEKUWA mbunge wa Kasarani Elizabeth Ongoro na mumewe Ferdinand Masha Kenga, huenda wakajipata mashakani huku Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) ikiwaangazia kuhusiana na Sh48 milioni.

Kulingana na taarifa ya EACC, iliyochapishwa Ijumaa kwenye mtandao wa kijamii wa Twitter, kandarasi ya pesa hizo zilizodhamiriwa kwa ujenzi wa Shule ya Upili ya Kasarani, ilikiuka sheria kuhusu ununuzi.

Aidha, EACC ilifafanua kuwa shule hiyo haikuwepo huku malipo ya fedha hizo yakitolewa kwa watu mbalimbali ikiwemo kampuni zinazomilikiwa na maafisa katika Hazina ya Maendeleo katika Maeneobunge (CDF)

“Tume ilibaini kuwa kutolewa kwa kandarasi ya ujenzi wa shule hiyo kulifanywa pasipo kuzingatia sheria kuhusu ununuzi. Shule hiyo haipo na malipo yalifanywa kwa watu tofauti na kampuni zinazohusishwa na msimamizi wa Hazina ya Serikali Kuu kuhusu Maendeleo ya Maeneobunge na wanakamati kwa huduma ambazo hazikutolewa,” ilisema EACC.

Kufuatia kukamilika kwa uchunguzi huo, Mwelekezi ya Mashtaka ya Umma (DPP) sasa ameamrishwa kukamatwa kwa watu 26.

Watakiwa kujiwasilisha

Bi Ongoro na mumewe pamoja na washukiwa wengine 17 wametakiwa kujiwasilisha kwa tume hiyo mara moja ili kuhojiwa.

Tume hiyo Ijumaa iliwakamata washukiwa wawili, Bw Kefa Omanga Omoi, aliyekuwa afisa wa Maendeleo Wilaya ya Kasarani na Jecinta Akoth Opondi aliyekuwa mwanachama wa CDF Kasarani, ambao watawasilishwa kortini.

Miongoni mwa mashtaka yanayowakabili ni pamoja na: kula njama za kutenda hatia ya ufisadi, usimamizi mbaya wa pesa za umma, matumizi mabaya ya afisi, kumiliki mali ya umma kwa njia haramu na mengineyo.

Haya yanajiri miaka minane baada ya Kenga kuripotiwa kukamatwa na kushtakiwa kuhusiana na wizi wa Sh1.9 milioni katika Benki ya Cooperative tawi la University Way.