Habari Mseto

Ongwae anaswa kuhusu mbolea feki, achunguzwa kwa sukari ya sumu

June 22nd, 2018 2 min read

Na CHARLES WASONGA 

MKURUGENZI Mkuu wa Shirika la Kukadiria Ubora wa Bidhaa (KEBS) Charles Ongwae Ijumaa alikamatwa kuhusiana na kashfa ya uingizwaji wa mbolea ghushi nchini huku shirika hilo likimulikwa kuhusiana na sakata ya sukari ya sumu.

Bw Ongwae alikamatwa pamoja na maafisa wengine wakuu wa shirika hilo, wale wa mamlaka ya ukusanyaji ushuru nchini (KRA) na wafanyabiashara kadhaa, watatu wakiwa raia wa Morocco.

Maafisa wa upelelezi pia wametoa ilani ya kukamatwa kwa wafanyabiashara wawili wanaosemekana kutorokea ng’ambo.

“Tumetoa ilani ya kukamatwa wa washukiwa wengine na tunashirikiana na polisi wa kimataifa kwa lengo la kuwakamata,” akasema Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) George Kinoti.

Maafisa wengine wakuu wa Kebs waliokamatwa na Ogwae ni mkurugenzi wa idara ya ubora Bw Eric Chesire na mwenzake wa idara ya ukaguzi Erick Ochieng’.

Mnamo Alhamisi Bw Ongwae na maafisa wengine wa shirika hilo walifika mbele ya kamati ya bunge kuhusu biashara ambapo walihojiwa kuhusu sukari iliyodaiwa kuwa na sumu.

Aliiambia kamati hiyo kwamba uchunguzi uliofanyiwa sukari ya magendo ulibaini uwepo chembechembe za madini ya shaba na chuma.

Hata hivyo, alisema chembechembe za madini ya zebaki (mercury) hazikupatikana katika sukari hiyo alivyodai Waziri wa Usalama Dkt Fred Matiang’i.

Uwepo wa viwango vya juu vya shaba na chuma ndani ya sukari unaashiria kuwa maisha ya mamilioni ya Wakenya yamekuwa yakitaharishwa kwani madini hayo husababisha matatizo mengi ya kiafya.

Wakati huo huo, waziri Matiang’i na wenzake Henry Rotich (Fedha), Mwangi Kiunjuri (Kilimo) na Adan Mohammed (Biashara) ni miongoni mwa maafisa wa serikali ambao watahojiwa na wabunge kuhusiana na sakata hiyo ya sukari Juni 25.

Wengine watakaofika mbele ya kamati ya pamoja ya Kilimo na ile ya Biashara ni Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Ukusanyaji Ushuru Nchini (KRA) John Njiraini, Inspekta Jenerali wa Polisi Joseph Boinnet, kiongozi wa wengi katika Bunge la kitaifa Aden Duale, miongoni mwa maafisa wengine.