Michezo

Onkar Rai, wengine sita wajiondoa duru ya KCB Kilifi Rally

August 17th, 2019 1 min read

Na GEOFFREY ANENE

BINGWA wa duru ya ufunguzi ya Mbio za Magari za Kitaifa za Kenya (KNRC) mwaka 2019, Onkar Rai ni mmoja wa madereva saba waliojiuzulu kufikia sasa kwenye duru ya KCB Kilifi Rally.

Onkar, ambaye alitwaa taji la KCB Nakuru Rally mwezi Februari, aliendelea kuandamwa na mikosi mwezi mmoja tu baada ya kujiuzulu katika duru ya Safari Rally ambayo pia ni ya Bara Afrika alipopata ajali.

Hajakuwa na bahati katika mashindano ya mbio za magari katika eneo la Pwani. Itakumbukwa Onkar alijiuzulu katika duru ya Mombasa Rally ya mwaka 2017, mwaka mmoja baada pia ya kuwa na mikosi katika KCB Wundanyi Rally.

Hata hivyo, Onkari alirejea Pwani akiwa na matumaini makubwa ya kufanya vyema baada ya kumaliza Mombasa Rally katika nafasi ya pili mwaka 2018 akiendesha gari lake la Skoda Fabia R5.

Katika Kilifi Rally mwaka huu, Onkar alishirikiana na mwekelezi wake Gareth Dawe.

Walijiuzulu katika mkondo wa pili wa mashindano (CS2). Madereva wengine ambao pia wako nje ya Kilifi Rally ni Piero Cannobio (Mitsubishi EVO10), Geoff Mayes (Land Rover), Adil Mirza (Mitsubishi EVO8), Raaji Bharij (Porsche 911), Hussein Malik (Mitsubishi EVO10) na Naushad Kara (Subaru Impreza).

Bingwa wa Afrika Manvir Baryan (Skoda Fabia) anaongoza Kifili Rally akifuatwa na Izhar Mirza (Mitsubishi EVO10), Tejveer Rai (Mitsubishi EVO10) na mshindi wa Safari Rally Baldev Chager (Mitsubishi EVO10) katika usanjari huo.

Mshindi wa Kilifi Rally, ambayo ni duru ya nne mwaka huu na ilivutia madereva 23, atajulikana baadaye leo Jumamosi jioni.