Siasa

Onya sana marafiki zako dhidi ya kushambulia Gachagua, Kahiga aambia Ruto


GAVANA wa Nyeri Mutahi Kahiga sasa anamtaka Rais William Ruto kuwadhibiti wandani wake anaodai wanaendelea kumshambulia naibu wake Rigathi Gachagua.

Gavana huyo alisema ni Dkt Ruto pekee ndiye mwenye uwezo wa kuwaamuru wanasiasa hao wamheshimu Bw Gachagua.

Kwenye mahojiano ya kipekee na runinga ya NTV Jumapili usiku, gavana huyo alisema inasitikisha kuwa Naibu Rais anashambuliwa na viongozi walio karibu na Dkt Ruto ilhali kiongozi wa taifa hasemi lolote.

“Namtaka Rais kutoa amri kwamba afisi ya Naibu Rais inapasa kuheshimiwa na mimi pia nitatii amri hiyo. Sio vizuri kwamba watu wanaomzingira ndio wale wanaomkosea heshima Gachagua,” akasema.

Naibu Rais amekuwa akishambuliwa kwa maneno kutokana na wito wake kwamba ugavi wa mapato ya serikali unapasa kufanywa kwa kuzingatia wingi wa watu katika maeneo mbalimbali nchini.

Lakini wandani wa Rais Ruto, wakiongozwa na kiongozi wa wengi katika Bunge la Kitaifa Kimani Ichung’wah wanamjibu kwamba mfumo huo utaendeleza ukabila na migawanyiko nchini Kenya.

Nao mawaziri wakiwemo Kithure Kindiki (Usalama), Moses Kuria (Utumishi wa Umma) na mwenzao wa Ulinzi Aden Duale wameungana na wanasiasa hao kumshambulia Gachagua kwa kuunga mkono mfumo huo wa ugavi wa mapato, maarufu kama “mtu-mmoja, kura-moja, shilingi-moja.”

SOMA PIA: Ruto amuomboleza Hakimu Kivuti muda mfupi baada ya kurejea nchini

Mbunge wa Kiharu Ndindi Nyoro na mwenzake wa Nyeri Mjini Duncan Mathenge pia ni miongoni kutoka eneo la Mlima Kenya ambao wanaendeleza vita dhidi ya Gachagua kutokana na msimamo wake kuhusu ugavi wa mapato.

Lakini wakati wa mahojiano katika NTV Gavana Kahiga, ambaye amekuwa mtetezi sugu wa Naibu Rais, alisema suala hilo limeingizwa siasa.

“Watu wanadhani tunaendeleza ubinafsi tunapopigia debe mfumo wa ‘mtu-mmoja, kura-moja, shilingi-moja’ lakini hiyo si kweli. Kile tunachotaka ni usawa. Mapato hutengewa watu na hilo ndilo suala ambalo tunahimiza. Nyeri yenye jumla ya watu 759,000 haitendewi haki chini ya mfumo wa sasa wa ugavi wa mapato. Kwa hivyo watu hawahisi kuwa serikali hii walioichagua inawahudumia ipasavyo,” Gavana Kahiga akasema.

Alimwonya Dkt Ruto kuwa huenda akapoteza uungwaji mkono kutoka Mlima Kenya ikiwa hatalishughulikia suala hilo.

Mnamo Jumamosi alipokuwa akihutubu akiwa Kutus, Kaunti ya Kirinyaga, Bw Gachagua aliyeonekana mwenye hasira aliwasuta watu fulani, ambao hakuwataja kwa “kujifanya wananiamuru”.

SOMA PIA: Hajutamaliza hata miaka miwili, afoka Gachagua akikemea siasa za urithi

“Shida iliyoko sasa ni kwamba watu ambao ni marafiki wa Rais wanataka kuwa mabosi wangu. Hiyo inawezekana kweli? Nashangaa kuwa hata wasaidizi wa kibinafsi wa Rais na mabloga wake wanataka kunielekeza. Wanataka kuniambia kile ambacho napasa kufanya. Wajue kuwa wao sio mabosi wangu,” Bw Gachagua akasema.

Aliongeza kuwa inasikitisha kuwa baadhi ya mawaziri na maafisa wanaoshikilia vyeo vya juu serikalini wanamhujumu badala ya kuelekeza juhudi zao katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

“Nimechaguliwa na watu wa Kenya na nina mabosi wawili, Rais na Wakenya. Kama wewe ni rafiki wa Rais, dumisha urafiki wako naye na ukome kuniingilia. Namfahamu bosi wangu na najua jina lake. Siwezi kushindwa kutofautisha bosi wangu na marafiki zake. Mimi sio mjinga, najua kutofautisha,” Bw Gachagua akasema.