Michezo

Onyango aanika azma kusaka cheo katika uchaguzi wa wanandondi

June 25th, 2019 1 min read

Na CHARLES ONGADI

MWENYEKITI wa Chama cha Ndondi Nchini (BAK) kaunti ya Kilifi, George Onyango ametangaza kuwa atawania kiti cha kitaifa cha naibu katibu mpanga ratiba.

Uchaguzi wa ndondi nchini unatarajiwa kuandaliwa katika uwanja wa kimataifa wa Kasarani jijini Nairobi mnamo Juni 28 mwaka huu ambapo Jamal Otieno amejitosa katika kinyang’anyiro cha uwaniaji wa kiti cha urais.

Onyango, ambaye ni mkufunzi mkuu wa klabu ya Malindi maarufu kama ‘Sting Sting ‘ inayoshiriki Ligi Kuu, amesema kwamba wakati umefika kwa mabadiliko katika mchezo huo nchini.

“Lengo langu kuu ni kuona mchezo huu unaoenziwa duniani umepata sura mpya kwa kusambazwa kila eneo nchini, “ alisema.

Onyango anajivunia kusambaza mchezo wa ndondi katika kila pembe eneo la Kilifi, huku akianzisha klabu kadhaa mjini Malindi.

Historia

Endapo Onyango atashinda, atakuwa afisa wa kwanza kutoka kaunti ya Kilifi kushikilia uongozi wa kitaifa wa mchezo huu nchini.

Wakati huo huo, mkondo wa tatu wa Ligi Kuu utaandaliwa mjini Mombasa kuanzia mwezi Julai kuanzia tarehe 18 hadi Julai 20.

Mkondo wa pili uliandaliwa mjini Busia mnamo mwezi Juni tarehe 13 hadi mwezi Juni tarehe 15 ambapo klabu ya Kenya Police almaarufu Chafua Chafua iliibuka na ushindi mkubwa. Mkondo wa nne unatarajiwa kuandaliwa Oktoba 24-26 mjini Nanyuki.