Michezo

Onyango alenga kurejea KPL kwa kishindo

September 15th, 2020 1 min read

CHRIS ADUNGO

STEPHEN Onyango aliibuka wa pili katika orodha ya wafungaji bora wa Ligi ya Kitaifa ya Supa (NSL) mnamo 2019-20, anatazamia kupata hifadhi mpya katika Ligi Kuu ya Kenya (KPL) katika muhula ujao wa 2020-21.

Onyango alisalia bila klabu mnamo Aprili baada ya kisa cha kwanza cha ugonjwa wa Covid-19 kuripotiwa humu nchini.

Fowadi huyo matata alitemwa na wanabenki wa KCB mnamo Januari na akarejea kambini mwa Fortune Sacco waliowapiku Nairobi City Stars na Nairobi Stima katika vita vya kuwania saini yake.

Hata hivyo, kipindi chake katika kikosi cha Fortune Sacco katika Kaunti ya Kirinyaga kilikuwa kifupi baada ya soka ya humu nchini kusitishwa kutokana na janga la corona mnamo Aprili.

“Maamuzi ya KCB kunitema yaliathiri pakubwa ndoto zangu za kuvunja rekodi ya miaka 14 ya ufungaji bora katika KPL (mabao 26) ambayo kwa sasa inashikiliwa na fowadi wa zamani wa Harambee Stars, Boniface Ambani,” akasema.

Ambani aliweka rekodi hiyo mnamo 2006 akivalia jezi Tusker baada ya kumfikia aliyekuwa nguli wa soka wa Gor Mahia, Maurice ‘Sonyi’ Ochieng aliyefunga magoli 26 mnamo 1976.

Onyango kwa sasa anafanya biashara ya kuuza mboga na matunda katika eneo la Githurai, Nairobi huku akitazamia kusajiliwa na kikosi cha KPL na kutangaza rasmi marejeo yake katika soka ya humu nchini.

“Japo sijapokea ofa zozote kufikia sasa, ninatazamia kwamba rekodi yangu ya awali katika NSL na KCB itanifanya kivutio kwa baadhi ya klabu za KPL kabla ya muhula wa usajili kufungwa rasmi,” akaongeza.

“Corona ilipobisha, hazina ya fedha ya Fortune ilitikiswa pakubwa na wakashindwa kulipa marupurupu na mishahara ya wachezaji,” akaongeza Onyango kwa kusisitiza kwamba alisalia kusugua benchi katika michuano mingi ya KCB licha ya kujitahidi zaidi mazoeni.