Makala

ONYANGO: Baringo sasa ni kitovu cha malaria, serikali iwe chonjo

September 1st, 2019 2 min read

NA LEONARD ONYANGO

SERIKALI ya Kaunti ya Baringo kwa mara nyingine imewasihi wahisani kujitokeza kukabiliana na mkurupuko wa maradhi ya malaria katika eneo hilo.

Watu wasiopungua 10 tayari wamefariki kutokana na maradhi hayo hatari ambayo huua maelfu ya Wakenya kila mwaka.

Malaria ni miongoni mwa maradhi makuu matatu yanayoua idadi kubwa ya Wakenya kila mwaka. Maradhi mengine ni nimonia na kansa.

Kwa mfano, ripoti kuhusu Hali ya Uchumi ya 2018 iliyotolewa na Shirika la Takwimu nchini (KNBS) ilionyesha kuwa, Wakenya 20,691 walifariki kutokana na malaria mnamo 201. Ugonjwa huo uliua watu 16,000 mnamo 2016 na 17,553 walifariki 2017.

Hiyo inamaanisha kuwa, Wakenya wasiopungua 48 hufariki kila siku nchini kutokana na malaria.

Hiyo si mara ya kwanza kwa Kaunti ya Baringo kukumbwa na mkurupuko wa malaria. Miaka miwili iliyopita, watu zaidi ya 20 waliaga dunia kutokana na maradhi hayo.

Maafisa wa afya katika kaunti ya Baringo tayari wamelalama kuwa barabara mbovu, ukosefu wa mtandao wa simu na uhaba wa vituo vya afya ni miongoni mwa changamoto kuu znazotatiza shughuli ya kuwafikia waathiriwa wa malaria, haswa katika vijiji vya Atirir, Kapau, Chesawach na Kutol.

Wagonjwa wanalazimika kusafirishwa umbali wa zaidi ya kilomita 100 kufikia kituo cha afya.

Maafa hayo yanayoshuhudiwa Baringo yangeepukika endapo serikali ya kaunti ingeweka mikakati madhubuti kukabiliana na malaria miaka miwili iliyopita.

Ukweli ni kwamba, ugonjwa wa malaria unasababishwa na mabadiliko ya hali ya anga. Mabadiliko ya hali ya anga yanasababisha joto kuongezeka duniani.

Kulingana na Shirika la Afya Duniani (WHO), mbu wanaoeneza ugonjwa wa malaria huzaana zaidi joto linapokuwa jingi.

Hiyo ndiyo maana maeneo yaliyo na joto jingi kama vile Nyanza na Pwani ndiyo yameorodheshwa na wizara ya Afya kuwa kitovu cha ugonjwa wa malaria.

Maeneo yaliyo na baridi kama vile sehemu za Bonde la Ufa na Kati zina maambukizi machache ya malaria.

Kwa kawaida, mabadiliko ya anga yamekuwa yakihusishwa na ukame ambao husababisha ukosefu wa chakula. Lakini ukweli ni kwamba, mabadiliko hayo huathiri zaidi sekta ya afya.

Sekta nyingine zinazoathiriwa na mabadiliko hayo ni miundomsingi, utalii, kilimo, usalama, viwanda, kawi nakadhalika.

Mabadiliko ya hali ya anga husabisha mambo mawili: mvua nyingi kupita kiasi ambayo huleta mafuriko au ukame unaosababishwa na ukosefu wa mvua.

Mvua nyingi kupita kiasi inaponyesha, miundomsingi kama vile barabara, madaraja na hata majengo huaribika. Maji mengi pia husababisha maradhi ya kipindupindu na hutoa maficho kwa mbu wanaosababisha malaria kuzaana.

Ukame husababisha uhaba wa maji na malisho hivyo kusababisha mapigano miongoni mwa jamii za wafugaji wa kuhamahama.

Serikali ya Kitaifa na Kaunti hazina budi kuweka mikakati ifaayo kukabiliana na athari hizi za mabadiliko ya hali ya anga.