Makala

ONYANGO: Chakula cha msaada kisiwe mtego, kitolewe bila masharti

April 30th, 2019 2 min read

Na LEONARD ONYANGO

WITO wa Gavana wa Turkana Josphat Nanok, kutaka serikali ya kitaifa kutumia chakula cha msaada kama chambo cha kuwanasa waathiriwa wa baa la njaa ili wajisajili na Huduma Namba, unafaa kushutumiwa vikali.

Kulingana na Gavana Nanok, chakula cha msaada kitawavutia watu zaidi ya 609,000 wanaokihitaji kwa dharura katika wadi zote 30 za Kaunti ya Turkana, kujitokeza kusajiliwa kupata Huduma Namba.

Wito huo wa Gavana Nanok si jambo geni humu nchini. Mabwanyenye wamekuwa wakitumia chakuka cha msaada kuwahadaa waathiriwa haswa wakati wa uchaguzi.

Miezi michache kabla ya Uchaguzi Mkuu wa 2017, Gavana Nanok alinukuliwa akishutumu wanasiasa wa Jubilee kuwa walitumia chakula cha msaada kushawishi wakazi wa Turkana ili kujipatia kura.

Kabla ya uchaguzi huo, serikali ilisambaza mawaziri wake katika maeneo mbalimbali ya nchi yaliyoathiriwa na baa la njaa kugawa chakula cha msaada kwa lengo la kuwashawishi wakazi kupigia kura upande wa serikali.

Tayari serikali imetangaza kuwa Huduma Namba inalenga kuwezesha Wakenya kupata huduma kwa haraka wanapoenda katika taasisi za umma.

Hivyo kila Mkenya hana budi kujitokeza na kujisajili ili aweze kufurahia huduma za serikali katika siku za usoni.

Hata hivyo, kutumia chakula cha msaada kama chambo cha kuwavuta waathiriwa wa njaa kujitokeza na kujiandikisha kwa ajili ya Huduma Namba, hakufai na ni ukiukaji wa Katiba.

Serikali inastahili kutumia njia mbadala kuhamasisha wakazi wa Turkana na maeneo mengineyo yaliyoathiriwa na baa la njaa na wala si kutumia chakula cha msaada.

Kifungu cha 43 cha Katiba kuhusu haki za Wakenya, kinasema kuwa kila mtu ana haki ya kukingwa dhidi ya njaa na anastahili kuwa na chakula cha kutosha.

Kifungu cha 53 kinasema kila mtoto ana haki ya kupewa lishe bora, makazi na afya njema. Katiba pia inasema kuwa ni jukumu la serikali kuhakikisha kuwa haki hizo zinatekelezwa.

Hiyo inamaanisha kuwa waathiriwa wa njaa wanafaa kushtaki serikali kwa kukosa chakula. Chakula cha msaada si hiari bali ni haki ya waathiriwa wa baa la njaa kulishwa na serikali.

Waathiriwa wa baa la njaa wanastahili kupewa chakula cha msaada bila kuwekewa masharti.