Makala

ONYANGO: Corona imefifisha zaidi umoja Afrika Mashariki

July 31st, 2020 2 min read

Na LEONARD ONYANGO

JANGA la virusi vya corona ambalo limetikisa ulimwengu limethibitisha kuwa Jumiya ya Afrika Mashariki (EAC) ingali dhaifu.

Janga hili pia limezua hofu kuwa programu nzuri kama vile mpango wa kutaka kuwa na sarafu moja ya Jumuiya ya Afrika Mashariki kufikia 2024 huenda ukasalia ndoto.

Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) Liberat Mfumukeko mapema mwaka 2020 alisema kuwa, mswada muhimu ambao ungewezesha mataifa ya Afrika Mashariki; Kenya, Rwanda, Tanzania, Burundi, Uganda na Sudan Kusini kutumia sarafu moja, tayari umetiwa saini na marais wa mataifa wanachama.

Mpango wa kutaka kuwa na sarafu moja ya EAC uling’oa nanga mnamo 2013 ambapo pande husika zilitia saini mkataba wa kuhakikisha kuwa ukanda wa Afrika Mashariki unatumia sarafu moja kufikia 2024.

Sarafu moja ililenga kurahisisha biashara na kuwezesha EAC kuwa na ushawishi katika ulingo wa kimataifa.

Mswada huo utawezesha kubuniwa kwa Taasisi ya Kifedha ya Afrika Mashariki (Eami) ambayo baadaye itabadilishwa kuwa Benki Kuu ya Afrika Mashariki.

Tangu kuzinduliwa upya miaka 20, EAC imekuwa ikikumbwa na misukosuko si haba.

Ukosefu wa fedha ya kuendeshea shughuli za jumuiya na mizozo miongoni mwa mataifa wanachama limekuwa jambo la kawaida.

Mnamo 2017, kiongozi wa Tanzania John Magufuli aliagiza kuteketezwa kwa vifaranga kutoka Kenya. Baadaye, Rais Magufuli alipiga mnada ng’ombe zaidi ya 1000 waliovuka mpaka na kuingia nchini Tanzania. Hatua hiyo ya Tanzania ilitikiza uhusiano wake wa kidiplomasia na Kenya.

Mataifa ya Uganda na Rwanda yamekuwa yakizozana kwa zaidi ya miaka miwili sasa kutokana na sababu za kisiasa. Rais Paul Kagame wa Rwanda amekuwa akidai kuwa mwenzake wa Uganda Yoweri Museveni ametoa hifadhi kwa waasi ambao wamekuwa wakihangaisha Kigali. Uganda, hata hivyo, imekanusha madai hayo.

Rais Kenyatta ambaye amekuwa akionekana kuwa kiongozi mpatanishi katika ukanda wa Afrika Mashariki pia atakuwa amestaafu kufikia 2024; hivyo huenda kiongozi atakayechukua hatamu za uongozi wa nchi hii akajikokota kuunga mkono juhudi za EAC kutaka kuwa na sarafu moja.

Burundi pia ina kiongozi mpya, Evariste Ndayishimiye, ambaye msimamo wake kuhusu EAC ungali haujulikani.

Lakini janga la virusi vya corona limekuwa chuma moto kwenye kidonda. Tangu janga la virusi vya corona kutua Afrika Mashariki, uhusiano baina ya Tanzania na Kenya umekuwa ukiyumbayumba. Uganda pia imekuwa ikihangaisha madereva wa malori wa Kenya na Tanzania.

Uganda imekuwa ikirejesha makwao Wakenya, watanzania na Wasudan Kusini wanaopatikana na virusi vya corona.

Janga la corona lilifaa kuunganisha mataifa ya jumuiya ya EAC lakini inasikitisha kuwa limesababisha utengano.