Makala

ONYANGO: EACC iadhibu wanasiasa wanaopuuza maagizo

July 27th, 2020 2 min read

Na LEONARD ONYANGO

WANASIASA wanaonekana kupuuzilia mbali agizo la Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) la kuwataka kukoma kuchapisha majina au picha zao kwenye bidhaa za misaada wanazonunua kwa kutumia fedha za umma.

Inaonekana wanasiasa wamechukulia onyo hilo la EACC kuwa sawa na kelele za chura ambazo haziwezi kumzuia ng’ombe kunywa maji.

Juni 2020 EACC ilitoa onyo kwa magavana, wabunge na MCAs dhidi ya kubandika picha au majina yao kwenye misaada wanayotoa kwa wananchi wakati huu wa janga la corona.

Tume hiyo ilisema kuwa wanasiasa wanaotaka kuchapisha majina au kubandika picha zao kwenye misaada, basi hawana budi kutumia fedha zao za kibinafsi.

Onyo hilo lilitolewa ya viongozi, haswa magavana na wabunge, kubandika picha zao kwenye misaada iliyonunuliwa kwa fedha za umma.

Kwa mfano, Gavana wa Nyeri Mutahi Kahiga alishutumiwa vikali kwa kubandika picha yake kwenye chupa za sanitaiza iliyokuwa imetolewa kama msaada na kiwanda cha sukari cha Kibos.

Mwakilishi wa Wanawake Kaunti ya Nairobi Esther Passaris, pia alikosolewa na Wakenya kwa kuweka picha yake kwenye sodo za bure kutoka kwa serikali kuu.

Lakini licha ya onyo la EACC, wanasiasa wanaendelea kusambaza misaada ya sanitaiza, barakoa, sabuni na vyakula iliyo na picha zao. Labda wanasiasa hao wanachukulia EACC kuwa sawa na jibwa lenye mazoea ya kubweka tu bila kung’ata.

Ili kuzima tabia hii, EACC inafaa kuanzisha uchunguzi dhidi ya wanasiasa wote ambao wamekuwa wakiweka picha na majina yao kwenye misaada na wanaopatikana na hatia waadhibiwe.

Kubandika picha kwenye miradi au bidhaa zilizonunuliwa kwa kutumia fedha za umma ni ufisadi wa kiwango cha juu na matumizi mabaya ya afisi.

Wanasiasa pia wamekiuka agizo la serikali la kuwataka kutotoa misaada moja kwa moja kwa wananchi ili kuzuia mikusanyiko ya watu ambayo inaweza kusababisha kasi ya kusambaa kwa virusi vya corona.

Vilevile, Shirika la Kudhibiti Ubora wa Bidhaa (Kebs) linafaa kuchunguza ubora wa sanitaiza, sabuni au barakoa ambazo zimekuwa zikisambazwa na wanasiasa.

Waziri Msaidizi wa Biashara Lawrence Karanja hivi karibuni alilalamikia kuhusu ongezeko la bidhaa feki kama vile sanitaiza, barakoa na sabuni, ambazo zimefurika nchini.

Kuna uwezekano hizi ndizo zimekuwa zikinunuliwa na wanasiasa na kusambazwa kwa wapigakura wao ili kujipatia umaarufu wa kisiasa.