Makala

ONYANGO: Fedha za wazee ziongezwe kukabiliana na makali ya njaa

April 25th, 2019 2 min read

Na LEONARD ONYANGO

SERIKALI imeanza shughuli ya kuondoa ‘walaghai’ ambao wamekuwa wakipokea Sh2,000 ambazo hutolewa kwa wazee wa umri wa miaka 70 na zaidi kila mwezi.

Kulingana na wizara ya Leba, hatua hiyo imechukuliwa baada ya Hazina Kuu ya kitaifa kubaini kuwa baadhi ya familia zimekuwa zikiendelea kupokea fedha hizo hata baada ya walengwa kuaga dunia.

Takwimu za wizara ya Leba zinaonyesha kuwa jumla ya watu 1.3 milioni, kati yao wakiwa wazee 523,000, wanapokea fedha hizo ambazo hutolewa kila baada ya miezi miwili.

Wengine wanaonufaika na fedha hizo kutoka kwa serikali ni watoto yatima na walemavu.

Japo hatua hiyo ya wizara kuondoa wazee waliofariki kutoka katika malipo hayo inafaa, mengi yanastahili kufanywa.

Humu nchini kuna zaidi ya wazee milioni mbili walio na umri wa miaka 70 na zaidi kwa mujibu wa hesabu za sensa ya 2009 iliyofanywa na Shirika la Takwimu nchini (KNBS).

Hiyo inamaanisha kwamba baadhi ya wazee hawanufaiki na fedha hizo licha ya kuwa na umri wa miaka 70 na zaidi.

Tangu kuanzishwa kwa malipo hayo, kumekuwa na malalamishi kwamba machifu na bodi za hazina za fedha kwa wazee wamekuwa wakiendeleza upendeleo.

Miaka miwili iliyopita, kundi la wazee kutoka Kaunti ya Migori walilamika kuwa bodi imekuwa ikiwapa kipaumbele wazee kutoka familia tajiri na kuwatelekeza maskini.

Wazee hao pia walilalama kuwa baadhi ya wajumbe wa bodi wamekuwa wakipokea hongo ili kuidhinisha majina ya baadhi ya wazee kupokea fedha hizo.

Wizara ya Leba haina budi kuchunguza madai ya kuwepo kwa visa vya ufisadi na upendeleo katika ugavi wa fedha za wazee.

Serikali inafaa kuhakikisha kuwa wazee wote waliofikisha umri wa miaka 70 wananufaika na fedha hizo kote nchini.

Kadhalika, serikali inastahili kuongeza mgawo huo maradufu kutoka Sh2,000 hadi Sh4,000 kila mwezi haswa katika wakati huu ambapo mamilioni ya Wakenya wanakabiliwa na baa la njaa.

Wazee na watoto ndio huathiriwa zaidi na makali ya njaa na kuongezwa kwa fedha hizo itakuwa njia mojawapo ya kukabiliana na makali ya njaa nchini.

Nyingi ya picha za waathiriwa wa njaa ambazo zimekuwa zikisambazwa katika mitandao ya kijamii, ni za wazee na watoto.

Kuna itikadi kwamba wazee husaidiwa na jamaa au watoto wao wanaofanya kazi. Lakini ukweli ni kwamba wengi wa wazee wanaishi maisha ya upweke na wametwika majukumu ya kulea wajukuu.

Tafiti pia zinaonyesha kuwa wazee wako katika hatari ya kupata maradhi wanapokosa chakula cha kutosha.