Makala

ONYANGO: Kanuni mpya za mikutano zisitumiwe kufinya wapinzani

October 10th, 2020 2 min read

Na LEONARD ONYANGO

TANGU Baraza Kitaifa la Ushauri wa Kiusalama (NSAC) kutangaza masharti makali kuhusu mikutano ya umma na kudhibiti uenezaji wa habari za ‘uchochezi’ kupitia mitandao ya kijamii, kumekuwa na mjadala mkali kuhusu ikiwa hatua hiyo ni ya kisiasa au la.

Wanasiasa wa mrengo wa Tangatanga ndani ya Jubilee, wanadai kuwa masharti hayo makali yanalenga kuzima kisiasa Naibu wa Rais William Ruto.

Mara baada ya Mkuu wa Watumishi wa Umma Joseph Kinyua kutangaza masharti hayo Jumatano, Dkt Ruto ambaye ni mmoja wa viongozi wakuu wanaoketi kwenye baraza la NSAC, alikuwa wa kwanza kuyakosoa.

Kulingana na Naibu wa Rais, wanasiasa wanafaa kuruhusiwa kufanya mikutano bila kuingiliwa na polisi.

Kwa mujibu wa masharti yaliyotangazwa na Bw Kinyua Jumatano na kuidhinishwa na Baraza la Mawaziri siku moja baadaye, watu wanaotaka kuandaa mikutano ya umma, wakiwemo wanasiasa, ni sharti wafahamishe wakuu wa polisi wa eneo husika siku tatu kabla.

Baraza Kuu la Usalama pia lilionya vyombo vya habari na watumiaji wa mitandao ya kijamii dhidi ya kusambaza taarifa zinazolenga kuzua uhasama kwa misingi ya kikabila.

Naibu wa Rais alikuwa wa kwanza kuhisi makali ya masharti hayo baada ya mkutano wake wa kuchangisha fedha uliofaa kufanyika Alhamisi katika Kaunti ya Nyamira kufutiliwa mbali na polisi.

Kulingana na polisi, Naibu wa Rais hakuwa na kibali kutoka kwa polisi kabla ya kuandaa mkutano huo.

Masharti hayo yanafaa kutuliza joto la kisiasa humu nchini ambalo limekuwa likipanda kila uchao licha ya kusalia miaka miwili kabla ya Uchaguzi Mkuu.

Wakenya waliathiriwa pakubwa na janga la virusi vya corona na wanahitaji mazingira shwari ya kufanyia biashara zao ili kujikwamua tena kiuchumi. Siasa za mapema hazifai.

Hata hivyo, masharti hayo yasitumiwe kugandamiza wanasiasa wanaopinga serikali.

Aghalabu serikali inapotoa masharti kama hayo hulenga kuyatumia kunyamazisha upinzani.

Mathalani, mnamo 2014, serikali ilishinikiza Bunge kupitisha sheria za usalama kwa lengo la kuzima upinzani ulioongozwa na kiongozi wa ODM Raila Odinga.

Baadaye, korti ilibatilisha vifungu kadhaa kwenye sheria hizo baada ya kubaini kuwa vilikiuka Katiba.

Vilevile, masharti hayo yaliyotangazwa na NSAC yasitumiwe kugandamiza uhuru wa kujieleza na kutangamana. Katiba inaruhusu watu kutangamana, kukutana na kujieleza bila uwoga.