Makala

ONYANGO: KNBS izuie wanasiasa wajeuri kuingilia sensa

July 23rd, 2019 2 min read

Na LEONARD ONYANGO

IDADI halisi ya Wakenya haijulikani licha ya serikali kufanya Sensa miaka 10 iliyopita. Hii ni kwa sababu baadhi ya maeneo yalijiongezea watu hewa.

Matokeo ya Sensa ya 2009 yalionyesha kuwa idadi ya watu katika maeneo ya Mandera, Wajir na Turkana ni milioni 2.35.

Baada ya kushindwa kuelezea walikotoka watu hao, aliyekuwa waziri wa Mipango wakati huo Wycliffe Oparanya mnamo 2012 aliwasilisha Bungeni idadi tofauti ambapo alisema maeneo hayo yalikuwa na watu milioni 1.3 milioni na wala si milioni 2.35.

Sensa ya 2009 ilifanywa kabla ya katiba ya 2010 ambayo imeleta mfumo wa ugatuzi.

Katika mfumo huu wa serikali za kaunti, visa vya udanganyifu kuhusu idadi ya watu huenda vikaongezeka. Hii ni kwa sababu kila kaunti inahitaji kupewa mgao mkubwa wa fedha kutoka kwa Serikali ya Kitaifa, na idadi ya watu ni miongoni mwa vigezo vikuu vinavyotumiwa kugawa fedha kwa serikali za kaunti.

Vigezo vingine ni kiwango cha umaskini, ukubwa wa eneo na miundomsingi.

Ni kwa sababu hii ambapo Kaunti ya Nairobi, Turkana, Bungoma, Kakamega kati ya nyinginezo hupata kiasi kikubwa cha mgao wa fedha kutoka kwa serikali ya kitaifa ikilinganishwa na kaunti zilizo na idadi ndogo ya watu kama vile Lamu.

Kwa mfano, katika bajeti ya mwaka wa matumizi ya fedha wa 2019/2020, Kaunti ya Nairobi, Turkana, Nakuru, Kilifi, Kakamega na Mandera zitapokea mgao wa zaidi ya Sh10 bilioni kila moja.

Nazo kaunti za Lamu, Elgeyo Marakwet, Tharaka Nithi, Laikipia na Taita Taveta zitapokea chini ya Sh6 bilioni kila moja.

Hivyo wanasiasa wa kaunti fulani huenda wakatumia ukora na kuongeza idadi ya watu ili waweze kujipatia mgao mkubwa.

Suala lingine ni kuwa matokeo ya Sensa itakayoendeshwa na Shirika la Takwimu nchini (KNBS) pia yatatumiwa na Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) kurekebisha mipaka ya maeneobunge na wadi.

Wanasiasa wakora pia watataka kuongeza idadi ya watu ili wadi zao zigawanywe na wawe madiwani katika uchaguzi wa 2022.

Kulingana na IEBC, shughuli ya kurekebisha mipaka ya wadi, maeneobunge na hata kaunti itangóa nanga mwaka ujao.

Hivi majuzi Mkurugenzi wa KNBS Zachary Mwangi alisema mwaka huu shirika hilo litatumia teknolojia ili kuzuia udanganyifu.

Kutumia teknolojia kisiwe kisingizio cha KNBS kuketi raha mustarehe wakingojea makarani kuhesabu watu na kisha kutuma matokeo. Hata uchaguzi mkuu hutumia teknolojia lakini husheheni visa tele vya wizi wa kura.

Shirika la KNBS linastahili kuwa macho ili kuhakikisha kuwa wanasiasa hawatumii ushawishi wao kuongeza idadi ya watu kwa manufaa yao ya kibinafsi.

Litakuwa jambo la kuaibisha ikiwa KNBS itatumia kiasi kikubwa cha fedha na kukusanya takwimu feki zilizosheheni ukora wa wanasiasa.