Makala

ONYANGO: Raila achunge sana asiwe mwathiriwa wa referenda

October 16th, 2018 2 min read

Na LEONARD ONYANGO

MJADALA kuhusu kuibadilisha Katiba kupitia kura ya maamuzi unazidi kuchacha huku idadi kubwa ya wanasiasa wakiunga mkono.

Wito huo ambao ulitolewa kwa mara ya kwanza na kiongozi wa ODM Raila Odinga umepingwa na baadhi ya wanasiasa wakiongozwa na Naibu wa Rais William Ruto wanaodai kuwa kiongozi huyo wa upinzani analenga kutumia Katiba kujipatia wadhifa wa waziri mkuu serikalini.

Bw Odinga alikuwa katika mstari wa mbele kupigia debe rasimu ya Katiba mnamo 2010 lakini yeye pia ni miongoni mwa waathiriwa walioonja makali ya Katiba hiyo.

Kwa mfano, wakati wa kampeni za kura ya maamuzi miaka minane iliyopita Bw Odinga alieleza Wakenya kuwa polisi wangepigia saluti washukiwa kabla ya kuwakamata.

Bw Odinga alisema Katiba ya 2010 ingalifikisha mwisho udhalimu wa maafisa wa polisi.

Lakini kiongozi huyu wa upinzani ndiye ameshuhudia udhalimu mkubwa wa polisi, haswa kabla ya uchaguzi uliopita.

Bw Odinga na viongozi wengine wa muungano wa NASA pamoja na wafuasi wao walitawanywa kwa vitoa machozi na hata kupigwa viboko na polisi wakati wa maandamano ya kutaka kuondoa afisini baadhi ya maafisa wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC).

Udhalimu wa polisi bado unaendelea kudhihirishwa dhidi ya Wakenya wanaoandamana kulalamikia haki zao. Madaktari, wauguzi, wanaharakati wa mashirika mbalimbali ya kijamii pia wamepokea vipigo kutoka kwa polisi wakati wa maandamano.

Udhalimu

Hivyo basi, Bw Odinga anapopigania mabadiliko ya Katiba ahakikishe kuwa udhalimu huo wa polisi unakomeshwa endapo kutakuwa na kura ya maamuzi.

Katiba ya 2010 ilifutilia mbali afisi kama vile za Kiongozi wa Upinzani na nyadhifa nyinginezo kama vile kuwania urais pamoja na ubunge kwa pamoja.

Katiba ya 2010 ilipoanza kutumika katika uchaguzi wa 2013, Bw Odinga aliambulia patupu na kujipata kwenye baridi ya kisiasa.

Bw Odinga alibandikwa ‘cheo’ cha kiongozi wa upinzani licha ya Katiba kutotambua afisi hiyo.

Kufikia sasa, Bw Odinga ambaye ana wafuasi zaidi ya milioni tano, yungali katika baridi ya kisiasa licha ya kukubali kushirikiana na Rais Uhuru Kenyatta.

Wanaounga mkono mabadiliko ya Katiba wahakikishe kuwa viongozi walio na uungwaji mkubwa nchini wanapata majukumu ya kutekeleza badala ya kutelekezwa kisiasa kama ilivyo kwa sasa.

Afisi ya kiongozi wa upinzani inafaa irejeshwe ili kumwezesha kiongozi aliyebwagwa katika urais lakini aliye na idadi kubwa ya wafuasi aweze kutekeleza majukumu ya kuchunguza serikali na kufichua sakata mbalimbali za ufisadi.

Afisi ya kiongozi wa upinzani inastahili kutengewa fedha za kutekeleza majukumu yake.

Mara hii Bw Odinga anapopigania mabadiliko ya Katiba achunge asije akajipata mateka wa mabadiliko hayo.