Makala

ONYANGO: Raila anavyochangia umaarufu wa Ruto kuongezeka

October 3rd, 2020 2 min read

Na LEONARD ONYANGO

UKARIMU wa Naibu wa Rais William Ruto ambapo anawapa vijana vifaa vya kufanyia biashara, zikiwemo wilbaro na mikokoteni, unazidi kuzua mjadala mkali humu nchini.

Baada ya kuonekana kutengwa na Rais Kenyatta, Naibu wa Rais amekimbilia kwa Wakenya wa tabaka la chini – ambao ni wengi – kutafuta uungwaji mkono.

Ili kukubalika, Dkt Ruto amekuwa akikutana na makundi ya vijana, wanawake, walemavu na viongozi wa makanisa na kuwashawishi kumuunga mkono 2022.

Naibu wa Rais tayari amejitwika jukumu la kuwa mtetezi na msemaji wa wanyonge, almaarufu hasla. Katika siku za hivi karibuni, Dkt Ruto ameonekana kuwa na uungwaji mkono katika maeneo mbalimbali ya nchi, ikiwemo eneo la Nyanza ambalo ni ngome ya hasimu wake wa kisiasa, Raila Odinga.

Umaarufu wa Dkt Ruto miongoni mwa walalahoi umekuwa ukiongezeka kila uchao, hali ambayo imeanza kuwatia tumbojoto wapinzani wake.

Bw Odinga pamoja na wanasiasa wanaomuunga mkono, wamekuwa wakipuuzilia mbali hatua ya Dkt Ruto kujitawaza kuwa mtetezi wa walalahoi.

Bw Odinga na washirika wake wanadai kuwa wilbaro au mikokoteni haziwezi kukwamua vijana kutoka katika lindi la umaskini ambalo limesababishwa na ukosefu wa ajira nchini.

Lakini ukweli ni kwamba Bw Odinga amechangia pakubwa katika kuongezeka kwa umaarufu wa Naibu wa Rais Ruto nchini.

Baada ya kutoroka upinzani na kugeuka kuwa ‘msemaji’ wa serikali ya Jubilee, umaarufu wa Bw Odinga ulianza kudorora.

Dkt Ruto alipotengwa serikalini alikimbilia kujaza pengo lililoachwa na Bw Odinga.

Raila alikuwa na wafuasi wengi, haswa katika maeneo yaliyotelekezwa kiuchumi, kwa sababu alionekana kuwa mtetezi wao.

Baada ya kujiunga na serikali, Wakenya maskini walikosa mtetezi na hiyo ndiyo maana wamempokea Dkt Ruto kwa mikono miwili. Huku Bw Odinga akijitwika ‘dhambi’ za Jubilee, Dkt Ruto amekuwa akijitakasa.

Hatua ya Dkt Ruto kukosa kongamano la kujadili janga la virusi vya corona lililofanyika Jumatatu katika Jumba la KICC ni mojawapo ya mbinu za Naibu wa Rais kujitakasa.

Kwa kuwa janga la virusi vya corona limehusishwa na sakata ya wizi wa fedha, Dkt Ruto huenda aliona kuwa kuhudhuria kongamano hilo kungetoa taswira kwamba ni miongoni mwa walionufaika na hela hizo.

Ili kuzima umaarufu wa Dkt Ruto miongoni mwa Wakenya walala hoi, Bw Odinga hana budi kuanza kukosoa serikali ya Jubilee. La sivyo, umaarufu wake utazidi kunyong’onyea na kufikia 2022 hatakuwa na ushawishi.

[email protected]