Makala

ONYANGO: Rais alifaa kuwa mstari wa mbele Siku ya Chakula Duniani

October 18th, 2019 2 min read

Na LEONARD ONYANGO

ULIMWENGU, siku mbili zilizopita, uliadhimisha Siku ya Chakula Duniani japo maadhimisho hayo yalionekana ‘kama vile’ yalipuuzwa humu nchini.

Baadhi ya Wakenya walichangamkia maadhimisho hayo kupitia mitandao ya kijamii kama vile Twitter na Facebook lakini wengi walikuwa wakifuatilia kwa karibu shughuli ya uzinduzi wa Reli ya Kisasa (SGR) kutoka Nairobi hadi eneo la Suswa (Kaunti ya Narok) iliyoongozwa na Rais Uhuru Kenyatta.

Wizara ya Kilimo pia ilionekana kutotilia maanani maadhimisho hayo.

Maadhimisho ya kitaifa yaliongozwa na Katibu wa Wizara ya Kilimo Hamada Boga kwenye Taasisi ya Mafunzo ya Kilimo ya Kwa Kathoka, katika Kaunti ya Makueni.

Hafla hiyo ilitatizika baada ya kuvamiwa na wanaharakati wa vuguvugu la GreenPeace Africa waliobeba mabango ya kuitaka serikali kuelekeza nguvu zake katika suala la uzalishaji wa chakula badala ya kusema tu bila kutenda.

Waziri wa Kilimo Mwangi Kiunjuri bila shaka alihudhuria hafla ya uzinduzi wa reli ya SGR.

Uzalishaji wa chakula cha kutosha nchini ni miongoni mwa nguzo kuu za maendeleo ambayo Rais Kenyatta ameahidi kutekeleza ili kukumbukwa na Wakenya atakapostaafu 2022.

Hivyo, ilitarajiwa kwamba Rais Kenyatta au Waziri Kiunjuri angetumia siku ya Oktoba 16, kuwaelezea Wakenya hatua ambazo serikali imechukua kuboresha sekta ya kilimo kuwezesha Kenya kuwa na chakula cha kutosha kufikia 2022.

Ripoti kuhusu hali ya chakula duniani ya 2019 iliyoandaliwa na Shirika la Chakula la Umoja wa Mataifa (FAO) inaorodhesha Kenya miongoni mwa mataifa yanayohitaji chakula kwa dharura.

Kulingana na ripoti hiyo, Kenya inakumbwa na uhaba wa chakula sawa nchi kama vile Sudan, Yemen, Zimbabwe, Jamhuri ya Afrika ya Kati (CAR) kati ya mataifa mengine ambayo yamekuwa yakikumbwa na machafuko ya mara kwa mara.

Ripoti ya FAO pia inaonyesha kuwa Kenya ni miongoni mwa nchi zaidi ya 30 za Afrika ambapo mamilioni ya watu wako katika hatari kubwa ya kukosa chakula.

Lishe bora

Kila Mkenya ana haki ya kupata lishe bora kwa mujibu wa Kifungu cha 43 cha Katiba. Kulingana na Katiba, kuwa kila Mkenya anafaa kulindwa dhidi ya makali ya njaa.

Mabadiliko ya tabianchi yamechangia katika kuzorota kwa uzalishaji wa chakula nchini kutokana na ukame au mafuriko yanayosababisha uharibifu wa mazao.

Inatabiriwa kuwa mavuno yataendelea kudorora kwa kiwango kikubwa kutokana na mabadiliko ya tabianchi.

Kando na changamoto hizo, ufisadi pia umekita mizizi katika sekta ya kilimo. Wakenya wangali hawajavuna matunda ya mradi wa unyunyiziaji maji wa Galana Kulalu licha ya walipa ushuru kutumia mabilioni.

Mabadiliko ya tabianchi, ufisadi na sera duni zimechangia katika uwepo wa njaa kila mwaka humu nchini.

Hivyo, tulitarajia serikali kutueleza hatua ambazo imechukua katika kuhakikisha kwamba Kenya inakuwa na chakula cha kutosha.