Makala

ONYANGO: Ripoti ya BBI haijatatua ukabila na usaliti wa kisiasa

October 24th, 2020 2 min read

Na LEONARD ONYANGO

RIPOTI ya Mpango wa Maridhiano (BBI) ni dhaifu na inafaa kufanyiwa mabadiliko kabla ya kuwasilishwa kwa Tume ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) kuanza mchakato wa kuandaa kura ya maamuzi.

Ripoti hiyo haijatatua tatizo la ukabila na kuzima usaliti wa kisiasa ambao umekuwa ukishuhudiwa kila uchao.

Vile vile, mapendekezo yaripiti yame mpa rais mamlaka kupindukia na huenda akayatumia vibaya.

Kukolea kwa ukabila, usaliti wa kisiasa na rais kutumia vibaya mamlaka huchangia pakubwa katika kutokea kwa uhasama wa kikabila humu nchini.

Kwa mfano, joto la kisiasa linaloshuhudiwa humu nchini sasa lilitokana na hatua ya Rais Uhuru Kenyatta kumhepa naibu wake William Ruto hata baada ya kumsaidia kushinda urais katika uchaguzi wa 2013 na 2017. Joto la kisiasa lililo nchini linasababishwa na hatua ya maafisa wa polisi kufanya kazi kwa upendeleo kwa kuhangaisha wanasiasa wa upinzani.

Kwa sasa rais hana mamlaka ya kutimua naibu wake, lakini Dkt Ruto ametengwa na anaonekana mgeni serikalini. Itakuwaje kwa waziri mkuu au makamu wa rais ambaye rais ana uwezo wa kuwatimua wakati wowote!

Ripoti ya BBI inapendekeza kuwa rais atamteua waziri mkuu siku saba baada ya kuapishwa.

Mtu anahitimu kuteuliwa kuwa waziri mkuu ikiwa ni mbunge na kiongozi wa chama au muungano ulio na idadi kubwa ya wabunge katika Bunge la Kitaifa.

Iwapo mtu huyo atakosa kuidhinishwa na zaidi ya nusu ya wabunge, ripoti hiyo inasema kuwa chama kilicho na idadi kubwa ya wabunge kitateua mwanachama mwingine. Mwanachama huyo akikataliwa na wabunge basi rais atateua mwanachama yeyote anayeamini atakubalika.

Waziri mkuu anaweza kutimuliwa na rais wakati wowote. Vile vile, ripoti haijasema kuwa ni sharti waziri mkuu atoke katika jamii tofauti na rais.

Kifungu hicho kina udhaifu. Ikiwa chama cha upinzani kitakuwa na idadi kubwa ya wabunge bungeni, lakini mwaniaji wake wa urais aibuke katika nafasi ya pili, inamaanisha kwamba chama hicho kitatoa waziri mkuu na kiongozi wa upinzani kwa wakati mmoja.

Vilevile, kulingana na mapendekezo ya ripoti, rais hajapigwa marufuku kutoteua waziri mkuu kutoka katika jamii yake.

Ripoti inafaa kufanyiwa marekebisho ili kuhakikisha kuwa Rais, naibu wa rais na waziri mkuu wanachaguliwa pamoja. Rais apokonywe mamlaka ya kumtimua Waziri Mkuu au Naibu wa Rais.

Kadhalika, rais, waziri mkuu na manaibu wake na makamu wa Rais watoke katika jamii tofauti.

Kwa kufanya hivyo, serikali itakuwa na sura ya taifa.