Makala

ONYANGO: Serikali haijawakinga kikamilifu watoto wanaonajisiwa

July 13th, 2020 2 min read

Na LEONARD ONYANGO

KATIKA siku za hivi majuzi, kumekuwa na mjadala mkali kuhusu ongezeko la idadi ya wasichana wanaopachikwa mimba maeneo mbalimbali nchini.

Ripoti iliyotolewa na Shirika la Amref Ijumaa ilifichua kuwa, zaidi ya wasichana 900 wanatiwa mimba kila siku Kenya. Kila mwaka, kwa mujibu wa ripoti hiyo, wasichana zaidi ya 13,000 huacha shule kutokana na mimba za mapema.

Ripoti zinaonyesha takribani wasichana 6,000 wamepachikwa mimba tangu shule zifungwemnamo Machi.

Hiyo inamaanisha wakati huu ambapo shule zimefungwa hadi 2021, idadi kubwa zaidi ya wasichana huenda wakakosa kurejea shuleni kutokana na ujauzito au ndoa za mapema.

Hali itakuwa mbaya zaidi iwapo kafyu ya kutotoka nje usiku itaondolewa na maeneo ya burudani kama vile baa kufunguliwa kabla ya wanafunzi kurejelea masomo yao mwaka 2021.

Lakini jambo la kusikitisha ni kwamba, serikali inaonekana kutolichukulia suala hilo kwa uzito.

Baadhi ya watumiaji wa mitandao ya kijamii pia wamelichukulia suala hilo kimzaha.

Rais Kenyatta wiki chache zilizopita alijitokeza na kulaumu machifu kutokana na ongezeko la wasichana wanaopata ujauzito wakati huu ambapo shule zimefungwa kufuatia janga la virusi vya corona.

Kulingana na Rais Kenyatta, machifu wamelaza damu na wameshindwa kuwalinda wasichana katika maeneo yao.

Rais wiki iliyopita, aliagiza machifu kuwasajili wasichana wanaopatwa na ujauzito ili wapate huduma za bure za matibabu katika hospitali za matibabu.

Isitoshe, anataka machifu kuwatambua wanaume wanaotekeleza uhalifu huo.

Kuwatishia machifu na kuwapa wasichana huduma za bure za kujifungua ni kazi bure iwapo wanaume wanaotekeleza uhalifu huo hawatasakwa na kuadhibiwa.

Kufanya mapenzi na msichana wa chini ya umri wa miaka 18 nchini ni kosa la jinai. Hivyo, wanaume wanaotekeleza uhalifu huo wanafaa kusakwa na maafisa wa polisi sawa na wahalifu wengine kama vile magaidi, wezi, nakadhalika.

Kuwatwika machifu mzigo wa kuwasaka wanaume wanaonajisi watoto ni ishara kwamba serikali inachukulia suala hilo kimzaha.

Kulingana na sheria, wanaume wanaonajisi watoto wa chini ya umri wa miaka 11 wanastahili kusukumwa jela maisha.

Wanaonajisi watoto wa kati ya umri wa miaka 12 na 15 wanastahili kifungo cha miaka 20 gerezani. Wanaotekeleza uhalifu sawa na huo kwa wasichana wa kati ya umri wa miaka 15 na 17 wanaadhibiwa kifungo cha miaka 15 gerezani.

Serikali isipochukulia suala hilo kwa uzito, Kenya huenda ikapiku Tanzania na Uganda kwa idadi kubwa ya wasichana wanaopachikwa mimba kila mwaka katika ukanda wa Afrika Mashariki..

Ripoti iliyotolewa mwaka jana na shirika la Save the Children, ilionyesha kuwa, wasichana 82 kati ya 1,000 wa umri wa miaka 15 na 19 hupachikwa mimba nchini Kenya.

Nchini Rwanda, kiwango cha wasichana wa umri sawa wanaopata ujauzito kwa kila 1000 ni 27, Burundi (27), Uganda (111) na Tanzania (117).