Makala

ONYANGO: TSC kuwaajiri walimu vibarua si suluhu tosha

October 8th, 2019 2 min read

Na LEONARD ONYANGO

HATUA ya Tume ya TSC ya kuwaajiri walimu 10,300 wa kibarua inafaa, ila si suluhisho la uhaba wa walimu nchini.

Kuna uhaba wa jumla ya walimu 125,000 katika shule za msingi na sekondari.

Shule za sekondari ambazo sasa zina wanafunzi wasiopungua milioni 2.8 zina upungufu wa zaidi ya walimu 95,000 huku shule za msingi zilizo na wanafunzi milioni 10 zikiwa na uhaba wa walimu 30,000.

Hivyo, hatua ya TSC kuwaajiri walimu wa kibarua 4,300 katika shule za msingi na wengine 6,000 katika shule za upili haitasaidia kumaliza uhaba uliopo.

Kulingana na TSC, walimu wa kibarua wa shule ya sekondari watalipwa mshahara wa Sh15,000 huku wenzao wa shule za msingi wakipewa Sh10,000.

Mshahara huo duni utakatwa kodi, kulingana na TSC.

Hiyo inamaanisha kuwa mwalimu wa shule ya upili huenda akasalia na takribani Sh12,000 huku mwenzake wa shule ya msingi akipokea Sh8,000. Fedha hizo ndizo atakazotumia kulipa kodi ya nyumba, umeme na kusaidia familia yake kujikimu!

Je, Sh8,000 zinaweza kumsaidia mtu vipi kujikimu, kwa mfano, jijini Nairobi, Kisumu, Mombasa na maeneo mengineyo ya nchi?

Huenda hiyo ndiyo sababu ya TSC kuamua kuajiri walimu wa kibarua wa umri usiozidi miaka 35 kama njia mojawapo ya kuhepa walio na familia!

Gharama ya maisha inaongezeka kila uchao hivyo mshahara huo ni mdogo mno; hautoshi kitu

Ili kuwatia motisha walimu hao wa kibarua, tume ya TSC inafaa kuongeza mshahara wao.

Walimu hao watafanya kazi kwa kipindi cha miezi 12 na kisha TSC itaamua ikiwa wataajiriwa kuwa walimu wa kudumu au la kwa kuzingatia utendakazi wao na uwepo wa hela.

Iwapo TSC haitakuwa na fedha za kuwaajiri kuwa walimu wa kudumu basi watarejea nyumbani na uhaba wa walimu utaendelea.

Serikali itenge fedha za kutosha

Serikali inafaa kutenga fedha za kutosha za kuajiri walimu wa kudumu badala ya kukimbilia njia za mkato.

Serikali inafaa kuipa elimu kipaumbele kwa kuajiri walimu wa kutosha.

Ni kinaya kwamba kila siku tumekuwa tukihimiza wanafunzi kutia bidii masomoni ilhali hakuna walimu wa kuwafundisha.

Ripoti iliyowasilishwa na TSC bungeni mwaka huu pia ilionyesha kuwa hakuna usawa katika ugavi wa walimu katika shule mbalimbali nchini.

Ripoti hiyo ilionyesha kuwa baadhi ya shule zina idadi kubwa ya walimu ilhali baadhi hazina walimu.

Kwa mfano, ripoti ilionyesha kuwa Kaunti ya Taita Taveta inahitaji walimu 2,151 wa shule ya msingi lakini kwa sasa kuna walimu 2,209. Hiyo inamaanisha kuwa kuna walimu 58 zaidi ilhali kaunti kama vile Kakamega, Migori na kadhalika hazina walimu wa kutosha.

TSC inafaa kuhakikisha kuwa kuna ugavi sawa wa walimu katika maeneo yote ya nchi.