Makala

ONYANGO: Tusiruhusu serikali kuongeza karo ya vyuo vikuu

December 5th, 2020 2 min read

Na LEONARD ONYANGO

WAKENYA wanafaa kupinga vikali jaribio la serikali kudhamiria kuongeza karo ya elimu ya vyuo vikuu.

Wizara ya Fedha na wakuu wa vyuo vikuu wanataka karo katika vyuo vikuu vya umma iongezwe kwa asilimia 200 kutoka Sh16,000 hadi Sh48,000 kwa mwaka.

Iwapo mpango huo utaidhinishwa, elimu ya vyuo vikuu itasalia kuwa ya wanafunzi kutoka familia za mabwanyenye huku maskini wakifungiwa nje.

Kulingana na wizara ya Fedha, hatua hiyo itasaidia vyuo vikuu kujikwamua kiuchumi baada ya kuathiriwa vibaya na makali ya janga la virusi vya corona.

Inaonekana kulingana na wakuu wa vyuo vikuu na maafisa wa wizara ya Fedha, mapato ya Wakenya yaliongezeka wakati wa janga la virusi vya corona!

Ni kinaya kwamba, huku serikali ikiongeza karo, Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (Helb) imepunguza fedha za mikopo ambayo imekuwa ikitoa kwa wanafunzi kutoka Sh45,000 hadi Sh37,000 kutokana na kile inachodai ukosefu wa fedha.

Hatua hiyo ya Helb ni pigo zaidi kwa wanafunzi kutoka familia maskini ambao wengi wao hutegemea pakubwa mikopo hiyo kulipa karo na kujikimu kimaisha wanapokuwa vyuoni.

Kwa kawaida, serikali hulipia wanafunzi wa vyuo vikuu Sh70,000 na wanafunzi hujilipia Sh16,000.

Iwapo pendekezo hilo litapitishwa, wanafunzi watajilipia Sh48,000 – kiasi ambacho ni zaidi ya Sh37,000 zinazotolewa na Helb.

Wakuu wa vyuo vikuu na wizara ya Fedha wanadai kuwa ongezeko hilo halitakuwa mzigo kwa wazazi kwa sababu huwa wanalipia watoto wao ada ya zaidi ya Sh50,000 katika shule za upili za bweni.

Wanadai kuwa wazazi pia hulipia watoto wao karo ya zaidi ya Sh30,000 katika vyuo vya kati.

Wanasema ikiwa wazazi wana uwezo wa kulipa zaidi ya Sh50,000 katika shule za upili kwa mwaka basi hawatashindwa kulipa Sh48,000 katika vyuo vikuu.

Wakuu wa vyuo vikuu na maafisa wa wizara ya Elimu wameajiriwa na wanajiweza kifedha na bila shaka watoto wao wanasomea katika shule za watoto kutoka familia za matajiri.

Hawajui masaibu ya Wakenya maskini wanaohangaika usiku na mchana kusaka cha kutia kinywani.

Ukweli ni kwamba idadi kubwa ya wanafunzi wanasomea katika shule za upili za kutwa kutokana na ukosefu wa fedha licha ya kupita vyema katika Mtihani wa Darasa la Nane (KCPE).

Wengi wa watoto kutoka familia maskini waliofanikiwa kujiunga na shule za upili zinazotoza ada ya zaidi ya Sh50,000 wanasomeshwa na wasamaria wema au wazazi wao walilazimika kuuza mashamba.

Pendekezo hilo la kutaka kuongeza ada ya vyuo vikuu linabagua watoto kutoka familia maskini na linafaa kutupiliwa mbali.

[email protected]