Makala

ONYANGO: Wakenya wote washirikishwe katika upanzi wa miti

December 30th, 2019 1 min read

Na LEONARD ONYANGO

MNAMO Julai 2019 Ethiopia ilivunja rekodi kwa kupanda miti milioni 350 kwa kipindi cha saa 12.

Miti milioni 200 ilipandwa katika maeneo 1,000 kote nchini humo.

Ethiopia ilivunja rekodi iliyokuwa ikishikiliwa na India baada ya kupanda miti milioni 50 mnamo 2016.

Mnamo 2016, aliyekuwa waziri wa Mazingira Judi Wakhungu alizindua mradi wa kutaka kupanda miti milioni tano kwa saa moja kwa lengo la kuvunja rekodi ya dunia.

Lakini mpango huo unaonekana ulisambaratika labda baada ya Bi Wakhungu kuondolewa katika wizara hiyo na kuteuliwa kuwa balozi wa Kenya nchini Ufaransa.

Kenya inalenga kupanda miti bilioni 2 kufikia 2022 kwa lengo la kuongeza eneo lenye misitu kutoka asilimia 7 hadi asilimia 10. Hiyo inamaanisha kuwa tunahitaji kupanda miti milioni 667 kwa mwaka katika kipindi cha miaka mitatu iliyosalia kabla ya 2022. Hiyo ni sawa na kupanda angalau miti 608,000 kwa siku. Kila Kaunti itahitaji kupanda miti 12,900 kwa siku.

Idadi hiyo ni kubwa iwapo serikali itaendelea na mbinu inayotumiwa sasa ambapo jukumu la kupanda miti litaachiwa Idara ya Huduma kwa Misitu (KFS), Shirika la Wanyamapori (KWS) na wizara ya Mazingira kati ya taasisi nyinginezo za serikali.

Jukumu la kupanda miti linafaa kuwa la Wakenya wote na wala halifai kuachiwa serikali tu.

Tabianchi

Madhara yanayosababishwa na mabadiliko ya tabianchi; kama vile mafuriko, mkurupuko wa maradhi na ukame hudhuru Wakenya wote.

Mashirika na kampuni za kibinafsi zinafaa kujiunga katika juhudi za upanzi wa miti.

Kampuni zinazojihusisha na upanzi wa miti zinafaa kupunguziwa ushuru.

Wanafunzi katika shule za umma na vyuo vikuu washirikishwe katika shughuli hiyo ya upanzi wa miti.

Kenya iige Ethiopia kwa kuandaa shindano la upanzi wa miti kwa lengo la kuvunja rekodi. Iwapo tutafanikiwa kupanda zaidi ya miti milioni 350 katika kipindi cha saa 12 na kuvunja rekodi ya Ethiopia basi tutakuwa tumepiga hatua kubwa ajabu.

Serikali ielimishe wananchi kuhusu umuhimu wa miti ili kila Mkenya afahamu uzuri wayo.