MakalaSiasa

ONYANGO: Wananchi washinikize magavana kutekeleza manifesto zao

May 22nd, 2019 2 min read

Na LEONARD ONYANGO

NI Wakenya wangapi bado wanakumbuka manifesto zilizotolewa na magavana, maseneta, wabunge au madiwani wao kabla ya uchaguzi wa 2017? Bila shaka ni wachache.

Asilimia kubwa ya Wakenya wanakumbuka tu Agenda Nne Kuu za Rais Uhuru Kenyatta; ambazo ni kuboresha huduma za afya kwa wote, utoaji wa nyumba nafuu, ustawishaji wa viwanda na kuwezesha nchi kuwa na chakula cha kutosha.

Kabla ya uchaguzi kila mwanasiasa aliyewania alikuwa na manifesto ilizosheheni ahadi tele.

Kabla ya uchaguzi wa Agosti 8, 2017, Gavana wa Nairobi Mike Sonko alitoa manifesto iliyokuwa na ahadi tele katika harakati za kutaka kumng’oa mtangulizi wake Dkt Evans Kidero.

Bw Sonko aliahidi kumaliza msongamano wa magari jijini Nairobi, kushughulikia uhaba wa maji, kudumisha huduma za afya, usafi na usalama, kubuni nafasi za ajira na kuhakikisha kuwa wafanyabiashara wadogo hawatozwi ushuru kati ya ahadi nyinginezo nyingi.

Lakini kufikia sasa ahadi hizo hazijatekelezwa. Hali ya usalama jijini imedorora katikati mwa jiji, vibanda vya wafanyabiashara wadogo alioahidi kutowatoza ushuru vimebomolewa na kuachwa wakihangaika, hospitali nyingi za kaunti hazina dawa za kutosha na hali ya usafi inatisha.

Katika manifesto yake, Gavana wa Kirinyaga, Ann Waiguru aliahidi kuhakikisha kuwa huduma za afya zinaboreshwa katika muda wa mwaka mmoja baada ya kuchaguliwa. Kufikia sasa Kirinyaga ni miongoni mwa kaunti ambapo huduma za afya zimedorora.

Gavana wa Kisumu Prof Anyang’ Nyong’o aliahidi kuhakikisha kuwa ukanda wa Ziwa Victoria unakuwa kivutio kwa wawekezaji. Kufikia sasa wavuvi wanaendelea kuhangaika baada ya magugu maji kuteka nyara Ziwa Victoria.

Mbali na magavana, wabunge, maseneta, wawakilishi wa wanawake na madiwani pia walitoa hadi tele kwa wananchi.

Badala ya kuendelea kungojea Rais Kenyatta kutekeleza Ajenda Nne, Wananchi hawanabudi kushinikiza magavana na viongozi wengine waliowachagua kutimiza manifesto zao.

Magavana wanapokea mamilioni ya fedha kutoa huduma muhimu kwa wananchi kama vile matibabu, utunzaji wa mzingira, kilimo kati ya nyinginezo.

Iwapo magavana watatumia fedha zao vyema tatizo la njaa litapungua kwa kiasi kikubwa.

Kuna haja ya Bunge kubuni sheria itakayowazuia magavana wanaokosa kutekeleza manifesto yao kuwania muhula wa pili.

Sheria hiyo itahakikisha kwamba wananchi wanafanyiwa waliyoahidiwa na kuondoa desturi ya wanasiasa kutoa ahadi hewa.