Makala

ONYANGO: Wauguzi wawe na vifaa vya kujikinga na virusi

April 5th, 2020 2 min read

Na LEONARD ONYANGO

HABARI kuhusu daktari aliyeambukizwa virusi vya corona na mgonjwa katika hospitali ya Ngara jijini Nairobi zinafaa kushtua Wakenya, haswa magavana.

Daktari huyo alibainika kuwa na virusi vya corona baada ya kutibu wagonjwa zaidi ya 100, kwa mujibu wa ripoti za vyombo vya habari.

Waziri wa Afya, Mutahi Kagwe, wiki iliyopita alithibitisha kuwa wahudumu 10 wa hospitali ya Ngara wanaoshukiwa kutangamana na daktari huyo tayari wametengwa.

Ikiwa kweli daktari huyo alihudumia zaidi ya wagonjwa 100, basi kuna haja ya kuwa na wasiwasi. Hospitali ya Ngara huhudumia watu wa mapato ya chini wanaoishi katika maeneo yenye msongamano mkubwa wa watu; hivyo ni rahisi kwa virusi hivyo kusambaa kwa kasi.

Katika siku za hivi karibuni, magavana wamekuwa wakijitokeza kwenye vyombo vya habari wakielezea mikakati ambayo wamechukua katika kuzuia maambukizi ya virusi vya corona.

Miongoni mwa mikakati iliyochukuliwa na baadhi ya magavana ni kubomoa vibanda vya wafanyabiashara maskini na kufunga masoko. Wengine wametenga vyumba kadhaa hospitalini vya kutenga watu wanaoshukiwa kuwa na virusi vya corona.

Lakini ukweli ni kwamba karibu kaunti zote hazijafanya lolote katika kuwanunulia wahudumu wa afya vifaa na mavazi ya kuwakinga dhidi ya virusi vya corona.

Inasikitisha kuwa hata katika hospitali zinazosimamiwa na serikali ya kitaifa pia wahudumu wa afya hawana vifaa na magwanda ya kuwakinga na virusi hivyo ambavyo vimeangamiza zaidi ya watu 55,000 kote duniani.

Kutia msumari moto kwenye kidonda, ripoti pia zinasema kuwa, baadhi ya madaktari na wauguzi wanaoshughulikia waathiriwa wa virusi vya corona pia wamelazimika kujinunulia vifaa vya kuwakinga wasiambukizwe virusi hivyo.

Madaktari huhudumia mamia ya watu kwa siku na endapo wataambukizwa virusi vya corona, basi watavisambaza kwa idadi kubwa ya wagonjwa.

Wagonjwa wakiambukizwa virusi vya corona basi uwezekano wao kupona ni finyu kwa kuwa wana kinga dhaifu za mwili.

Takwimu zinaonyesha kuwa, wengi wa wanaokufa kutokana na virusi vya corona wana matatizo mengineyo ya kiafya kama vile kifua kikuu (TB), Ukimwi, saratani, nakadhalika.

Badala ya kubomoa vibanda vinavyotumiwa na maskini kutafutia riziki familia zao, magavana wanafaa kuhakikisha kuwa wahudumu wa afya katika hospitali zote wanapewa vifaa na mavazi ya kuwakinga na virusi vya corona.

Ni wazi kwamba, huduma za matibabu katika hospitali mbalimbali za kaunti zimekwama kwa kuwa madaktari wamekuwa wakiwarejesha nyumbani wagonjwa kutokana na kigezo kwamba hawana vifaa vya kuwakinga.

Hali ikiendelea hivi, Kenya huenda ikapoteza idadi kubwa ya watu watakaofariki kutokana na magonjwa mengineyo yanayoweza kutibika.

Itakuwa kazi bure kuelekeza nguvu zote katika kukabiliana na virusi vya corona ilhali maelfu ya watu wanakufa kutokana na maradhi mengineyo.