Michezo

Onyesha ubabe wako kitandani, Firmino aambiwa na mkewe

June 25th, 2020 1 min read

Na CHRIS ADUNGO

LARISSA Pereira ambaye ni mkewe mshambuliaji wa Liverpool na timu ya taifa ya Brazil, Roberto Firmino, sasa amelitaka dume lake kufanya hima na kumpa mtoto wa tatu atakayelikomaza zaidi penzi lao.

Firmino, 28, alifunga pingu za maisha na Larissa mnamo Julai 2017 katika sherehe za harusi iliyoandaliwa viungani mwa mji wa Maceio, Kaskazini mwa jiji la Alagoa, Brazil.

Wawili hao ambao hadi kufikia sasa wamejaliwa watoto wawili wa kike, walikula yamini ya ndoa baada ya kuchumbiana kwa takriban miaka minne.

Walifunga pingu za maisha mbele ya umati uliomjumuisha pia mamaye Firmino, Mariana Cicera, Philippe Coutinho, Lucas Leiva na Allan Souza na wanasoka mahiri wa zamani katika vikosi vya Liverpool na Brazil.

Wiki jana, Larissa alipakia mitandaoni picha za utata zilizowazingua wengi wa mashabiki wake kwenye mtandao wa Instagram. Katika mojawapo ya picha hizo, kipusa huyo alikuwa akirusha roho na Firmino katika ufuo wa Ibiza, Uhispania.

Kidosho huyo alikuwa amevalia rinda fupi la rangi ya bluu na kushikilia shada la maua mekundu yaliyounda umbo la moyo kuashiria upendo wake kwa Firmino.

Mwishoni mwa mwaka jana, Firmino alilazimika kuchanja chale zenye mchoro wa jina la mkewe kifuani pake ili kudhihirisha ukomavu wa penzi lake kwa Larissa.

“Nina kiu ya kukuzalia mtoto mwingine. Mpenzi fanya hima unifunge bao kabambe la penzi nihisi raha ya kuitwa mama kwa mara nyingine,” akaandika Larissa.