Makala

Onyesho la 'Sarafina' lafufua kituo cha uigizaji Nakuru

March 24th, 2020 3 min read

NA RICHARD MAOSI

Kadri nyota za waigizaji wa Hollyhood na wale wa Afro Sinema zinavyozidi kupata ufanisi, Nakuru Arts Theatre inaendelea kudidimia kutokana na idadi ndogo ya wasanii chipukizi wanofika ukumbini hapo kujiongezea tajriba.

Kulingana na uchunguzi uliofanywa na Taifa Leo Dijitali kupitia mazungumzo na baadhi yao , ni wasanii wachache ambao vilevile wamejitwika jukumu zito la kutangaza mchango wa jukwaa hili kwa uchumi wa kaunti ya Nakuru.

Wengi wao wakiwa ni wanafunzi wa vyuo vikuu, na wengine kutoka kwenye taasisi ya vyuo vya kiufundi anuwai pamoja na mashiriki ya kibinafsi yanayojihusisha na sanaa ya maigizo ya jukwaani,wakati wao wa mapumziko.

Aidha Nakuru Arts Theatre imemudu kutengeneza nafasi za ajira kwa baadhi ya vijana wanaotamba katika kipindi cha Churchil Show, kama vile Profesa Hamo na Dj Shitty anayeigiza katika kipindi cha Househelps of Kawangware.

Siku za mbeleni ukumbi wa Nakuru Arts Theatre ulitumika na mabwenyenye enzi za ukoloni kama vile Lord Egerton na Lord Delamere kupitiza muda wao wakati wa kutafuta burudani.

Mbali na mapenzi ya watu kwa sanaa ya maigizo ya jukwaani, wakazi wa Nakuru wanasema linaendelea kupoteza ubora kutokana na miundo misingi duni, ambayo imepitwa na wakati, huku baadhi ya mijengo zaidi ya karne moja iliyopita ikiwa imesimama.

Nakuru Arts Theatre ilirekebishwa mnamo 1949 baada ya kuta kutengeneza michirizi ya nyufa, katika pande zote na mabati kuzama, mjengo ulipozidi kuchakaa.

Mmoja wa wakurugenzi wake Joseph Maina anasema hali hii ilikuwa mbaya kwa sababu iliashiria kuwa sanaa ilikuwa inaelekea kuzama, akisema angalau serikali ya ugatuzi imejizatiti kurejesha hadhi yake, ingawa sio kwa asilimia mia moja.

“Hivi sasa tumepata vyombo vya kisasa ambavyo vimebadilisha taswira ya ukumbi wenyewe, ambao mara nyingi unatumika na wasanii kufanyia mazoezi kuanzia Jumatatu hadi Jumapili kila wiki,”akasema.

Alieleza kuwa mabati yamekarabatiwa, viti kurekebishwa na kuta zote kupakwa rangi na hali hii imerejesha uhai na mwonekano wa kuvutia, huku akisema malango yake yako wazi kwa wageni.

Mbali na waigizaji na waimbaji wanaotembelea jukwaa hili, wanafunzi wa vyuo vikuu, shule za msingi , upili na wasomi wamekuwa wakifanya utafiti ndani ya mjengo huu wenye maktaba na vitabu vya kale, ambavyo vimehifadhi asasi za kijamii na historia ya mabeberu.

“Baada ya kumaliza kidato cha nne sikua na jambo la kufanya ndiposa rafiki yangu mmoja akanishauri niendeleze kipaji changu cha uimbaji Nakuru Arts Theatre,”anasema Veryl Akinyi ambaye ni mwimbaji wa muziki wa kufokafoka.

Veryl ameporomosha vibao kadhaa kama vile ,sina Taabu, ambapo siku za mbeleni analenga kupata lebo yake na kuwavutia wasanii chipukizi wanaokumbana na changamoto wakati wa kutafuta maprodusa.

Taifa Leo Dijtali ilipotembelea ukumbi wenyewe iliwakuta baadhi ya vijana wakifanya mazoezi ya kuigiza vitabu vya fasihi kwa shule za upili, vitabu vya kiada katika silabasi ya shule ya msingi na upili

Kundi lenyewe linalofahamika kama Skynet limekuwa likizuru shule za upili kote nchini kuwatumbuiza wanafunzi kupitia maigizo ya jukwaani, ambayo hutahiniwa katika mitihani ya kitaifa KCSE.

Kwa upande mmoja mwigizaji Catherine Obare anasema mwonekano mpya wa jukwaa hili tayari umesha kuonyesha dalili za mafanikio miongoni mwa vijana wenye ari ya kujiendeleza katika jukwaa la sanaa.

Catherine anaamini kuwa Nakuru Arts itakuja kufikia kiwango cha kimataifa endapo serikali itatilia maanani umuhimu wa kazi za sanaa.

Aidha Nakuru Arts imesaidia kukuza maadili miongoni mwa vijana wanaomiminika jukwaani kila siku za wiki kujishughulisha badala ya kushinda nyumbani wakitazama filamu.

Anaamini kuwa wizara ya elimu na ile ya michezo, itawekeza katika sanaa ili kupanua uga wa kufundisha vijana wa kesho namna ya kujitegemea, badala ya kusubiri kazi za kuajiriwa.

Mnamo Octoba 23 , 2019 ukumbi wa Nakuru Arts Theatre ulianza kupata mashiko baada ya mchezo wa SARAFINA,kuigizwa kwa mara ya kwanza humu nchini, mjini Nakuru.

Waigizaji kutoka Nakuru, walipata nafasi ya kutangamana na wale wa Nairobi angalau kuonyesha upeo wao wa tajriba, huku wakiwa wamevalia magwanda maalum ya kusakata densi walisimamisha shughuli katika barabara ya Kenyatta kutwa nzima.

Waziri wa michezo, sanaa na michezo kutoka kaunti ya Nakuru Bi Abduba Tume alisifia hatua ya maonyesho hayo kuletwa mjini Nakuru hasa wakati huu ambapo, Nakuru Arts Theatre inaadhimisha miaka 70 tangu ianzishwe.

Aliongezea kuwa kupitia sanaa, ukumbi wa Nakuru Arts umefanikiwa kuajiri zaidi ya vijana 40 wanaofanya kazi katika vitengo mbalimbali kama vile kupiga picha, kulainisha sauti, kutahini wanamuziki na wanamitindo.

Nakuru Arts Theatre ilifanywa kuwa ukumbi rasmi mwaka wa 1958, baada ya juhudi za muda mrefu kutoka kwa washika sau waliokuwa na maono ya kudumu katika ulingo wa sanaa.