Onyo kwa makanisa yakome kuombaomba pesa za wanasiasa

Onyo kwa makanisa yakome kuombaomba pesa za wanasiasa

Na DAVID MUCHUI

BARAZA kuu la Makanisa nchini Kenya (NCCK) limewataka wachungaji kukoma kuombaomba michango kutoka kwa wanasiasa ili kuepuka kutumika kwa makanisa kama majukwaa ya kueneza matusi na siasa chafu.

Kamati ya NCCK katika tawi la Mashariki ya Juu ikiwemo Tharaka Nithi, Meru, Isiolo na Marsabit limewaonya wachungaji dhidi ya kuwapa wanasiasa nafasi ya kupiga siasa makanisani.

Onyo hili limetolewa wakati ambapo wanasiasa wengi wamekuwa wakilenga makanisa kupitia michango ili kujipendekeza kabla ya uchaguzi mkuu wa 2022.

Akizungumza baada ya mkutano mjini Meru, mwenyekiti wa kamati ya eneo la Mashariki ya Juu, Askofu Jediel Kaigongi alisema makasisi wanafaa kulinda madhabahu dhidi ya wanasiasa wenye ndimi kali.

“Msimpe mtu yeyote nafasi ya kupiga siasa na kuongea lugha chafu kanisani. Makanisa yanafaa kuwa maeneo teule ambapo kila mtu anaweza kumuomba Mungu.

Kamati hii inawaomba viongozi wa dini kuepuka michango kutoka kwa wanasiasa. Unapowaomba misaada ya kifedha, wanatumia nafasi hiyo kufanya siasa chafu na ya utengano makanisani,” Askofu Kaigongi alionya.

Alisema kuwa makanisa yanafaa kufanya bidii ili kujiweka huru kifedha kusudi wasitegemee misaada ya wanasiasa.

Kuhusu mchakato wa kubadilisha katiba ulioanzilishwa na Mpango wa Maridhiano (BBI), kamati hiyo ya NCCK imeitaka serikali kuhakikisha kuwa kila Mkenya amehusishwa kikamilifu.

“Kamati ya eneo la Mashariki ya Juu inawaomba Wakenya kuimarisha amani sasa, wakati wa kura ya maamuzi na baadaye. Kusiwe na Mkenya yeyote atakayeumizwa au kufa kwa sababu ya kura ya maamuzi,” Askofu akasema.

Kiongozi huyo wa kidini aliongeza kuwa makanisa ya eneo hilo yatatangaza na kumwaibisha mwanasiasa yeyote atakayechochea vurugu wakati wa kampeni.

Aidha, NCCK imewaomba Wakenya kufanya maamuzi huru wakati wa kura ya maamuzi.

“Msiwakubali wanasiasa kuwafanyia uamuzi kwa sababu wanapigania haja zao. Msikubali hongo ili kubadilisha msimamo wenu,” alishauri.

Baraza hilo la muungano wa makanisa pia limevitaka vitengo tofauti vya serikali kuchukulia hatua ya haraka yeyote atakayeendeleza siasa ya chuki.

Wakati huo huo, askofu mkuu wa Kanisa la Kimethodisti Joseph Ntombura amewashauri wakenya kutopotoshwa na wanasiasa wanapong’ang’ania umaarufu.

Askofu Ntombura alisema badala yake, Wakenya wanafaa kusikiliza na kutazama yanayoendelea na baadaye kufanya uamuzi bila kushurutishwa.

Aidha, aliwaomba Wakenya kuwakaribisha wanasiasa wote katika maeneo yao na kuepuka matendo yanayoweza kuvuruga amani.

You can share this post!

Wakala akana kuiba Sh11 milioni za bima

Messi afunga mabao mawili na kusaidia Barcelona kupepeta...