Habari

Onyo kwa waundaji wa filamu bila leseni

May 15th, 2018 1 min read

Na LEONARD ONYANGO

BODI ya Kutathmini Ubora wa Filamu nchini (KFCB) imetishia kuwashtaki watengenezaji wa filamu wanaohudumu bila vibali, huku ikitoa makataa ya siku 14 kwao kujitokeza kuchukua leseni.

Mkurugenzi Mkuu wa KFCB Ezekiel Mutua Jumatatu alisema bodi hiyo itaanzisha msako wa kuwanasa watengenezaji wa flamu wanaohudumu kinyume cha sheria baada ya kukamilika kwa makataa hayo.

Kulingana na Kifungu cha 4 (1) cha Sheria kuhusu Utengenezaji wa Filamu, watengenezaji wa filamu zinazonuiwa kuonyeshwa kwa umma ni sharti waidhinishwe na bodi ya KFCB.

Sheria hiyo pia inapendekeza faini ya fedha zisizozidi Sh100,000 au kifungo kisichozidi miaka mitano gerezani au adhabu zote mbili kwa watengenezaji wa filamu wanaopatikana na hatia ya kuhudumu bila idhini.

Kifungu cha 34 cha sheria hiyo pia kinasema kuwa ikiwa shirika, kampuni au chama kitakiuka sheria hiyo maafisa wasimamizi wake watawajibika.

“Bodi imebaini kuwa baadhi ya watengenezaji wa filamu wa humu nchini na kimataifa wamekuwa wamekuwa wakihudumu bila leseni. Kwa hiyo bodi ingependa kuwafahamisha kuwa kutengeneza filamu za kutazamwa na umma bila kibali kutoka kwa KFCB ni haramu,” akasema Dkyt Mutua.

Bodi ya KFCB ndiyo imetwikwa jukumu la kutathmini ubora wa filamu kabla ya kupeperushwa au kusambazwa kwa lengo la kuwalinda watoto dhidi ya kuonyeshwa filamu hatari na zinazokiuka maadili ya kijamii.

“Kwa hiyo bodi imetoa makataa ya siku 14 kwa watengenezaji wa filamu ambao hawajaidhinishwa kujitokeza na kuchukua leseni la sivyo watachukuliwa hatua za kisheria baada ya kukamilika kwa makataa hayo,” akasema Dkt Mutua.

Mwaka 2017, KFCB iliwataka watengenezaji wa filamu walioidhinishwa na bodi hiyo kutolipa ada zozote kwa serikali za kaunti.

Dkt Mutua alisema shughuli ya usimamizi wa filamu haikugatuliwa hivyo ni jukumu la serikali ya kitaifa.

“Mtengenezaji wa filamu anapopata leseni kutoka kwa KFCB hafai kwenda kutafuta kingine kutoka kwa serikali ya kaunti. Bodi ya KFCB iko tayari kuingilia kati kuhakikisha kuwa kaunti zinazohangaisha watengenezaji walioidhinishwa zinafikishwa mahakamani,” akasema Mkurugenzi Mkuu.