Onyo la Man City kwa wapinzani wao Uefa

Onyo la Man City kwa wapinzani wao Uefa

MANCHESTER, Uingereza

Na MASHIRIKA

Manchester City ilidhihirisha ina ukatili wa kuwania taji la Klabu Bingwa Ulaya baada ya kuzima Paris Saint-Germain iliyokuwa na masupastaa Lionel Messi, Kylian Mbappe na Neymar 2-1 ugani Etihad na kutinga mduara wa 16-bora Jumatano.

City, ambayo ni timu ya nne ya Uingereza kuingia awamu hiyo ya muondoano msimu huu baada ya Liverpool (Kundi B), Chelsea (Kundi H) na Manchester United (Kundi F), ilituma onyo hilo kwa wapinzani wengine kwa kuzamisha PSG kupitia mabao ya Raheem Sterling na Gabriel Jesus.

Katika mechi hiyo ya Kundi A, ambayo City ilijibwaga uwanjani ikijivunia rekodi ya kulemea PSG mara tatu na kutoka sare katika historia yao ya Klabu Bingwa, iliona lango kupitia kwa Mbappe dakika ya 50. Mbappe alikuwa akishiriki mchuano wake wa 50 kwenye Klabu Bingwa.

Alikamilisha shambulizi lililopikwa na Neymar na Messi. Hata hivyo, Sterling alisawazisha kutokana na krosi ya Kyle Walker dakika ya 63 kabla ya Jesus kumwaga kipa Keylor Navas baada ya kupokea pasi safi kutoka kwa Bernardo Silva dakika ya 76.

Ushindi huo uliweka City ndani ya 16-bora kwa mwaka wa tisa mfululizo. PSG pia ilisonga mbele baada ya kunufaika kwa Leipzig kukung’uta Club Brugge 5-0.“PSG ni kali. Tulijitahidi kuzuia washambuliaji wao kufika maeneo yetu hatari kwa sababu wanaweza kufanya lolote wakikaribia lango.

Tunafurahi sana kuingia awamu ijayo,” alisema kocha Pep Guardiola aliyekosa huduma za wachezaji wabunifu Kevin De Bruyne, Jack Grealish na Phil Foden.Kocha Mauricio Pochettino anayemezewa mate na Manchester United baada ya Ole Gunnar Solskjaer kutimuliwa, alisikitika vijana wake wa PSG kupigwa.

Timu nyingine zilizofuzu Jumatano ni Real Madrid na Inter Milan.Washikilizi wa mataji mengi ya Klabu Bingwa, Real Madrid (13) walifuzu kushiriki awamu ya muondoano kwa mwaka wa 25 mfululizo kwa kunyamazisha Sheriff Tiraspol 3-0 nchini Moldova.

David Alaba, Toni Kroos na Karim Benzema walifungia viongozi hao wa Kundi D.Edin Dzeko alipachika magoli yote ya Inter ikibwaga Shakhtar Donetsk 2-0. Wengine ndani ya 16-bora ni Ajax na Sporting Lisbon (Kundi A), Bayern Munich (Kundi E) na Juventus (Kundi H).

Barcelona ama Benfica (Kundi E), Villarreal ama Atalanta (Kundi F), Porto, Atletico Madrid ama AC Milan (Kundi B) na Lille, Red Bull Salzburg, Lille, Wolfsburg na Sevilla (Kundi G) wangali na nafasi kubwa ya kuzoa tiketi tano zilizosalia kutoka makundi hayo yao.

You can share this post!

Shujaa mawindoni kulipiza kisasi Dubai 7s msimu mpya...

Wazalendo yazuru Accra kushiriki mashindano ya hoki Klabu...

F M