Habari Mseto

Onyo mvua kubwa kunyesha siku 4 zijazo

April 18th, 2020 1 min read

Na COLLINS OMULO

IDARA ya Utabiri wa Hewa nchini imewaonya Wakenya kujitayarisha kwa mvua kubwa kwa siku nne zijazo, ambayo huenda ikasababisha mafuriko na maporomoko ya ardhi.

Hilo linajiri baada yake kusema kuwa, mvua inayonyesha katika sehemu mbalimbali nchini itaendelea wikendi hii na mapema wiki ijayo.

Idara ilisema kuwa mvua hiyo inatarajiwa kunyesha katika maeneo ya Magharibi, Kati, Nairobi na Pwani.

Maeneo ambayo huenda yakaathiriwa sana ni kaunti za Kwale, Kilifi, Mombasa, Lamu, Tana-River, Taita Taveta, Nairobi, Nyeri, Kiambu, Nyandarua, Murang’a, Embu, Meru, Kirinyaga, Tharaka Nithi, Isiolo na Samburu. Kaunti zingine ni Turkana, Machakos, Kitui, Makueni, Garissa, Busia, Kisii, Nyamira, Kericho, Bomet, Nakuru, Narok,Migori, Trans Nzoia, Nandi, Pokot Magharibi, Baringo, Uasin Gishu, Elgeyo Marakwet, Vihiga, Bungoma, Homa Bay, Kisumu, Siaya, Kakamega na Nakuru.

Hivyo, watu wanaoishi katika maeneo hayo wameshauriwa kuwa waangalifu, hasa dhidi ya maeneo ambayo huenda yakakumbwa na mafuriko.

Baadhi ya maeneo hayo ni yale yaliyo karibu na milima ya Aberdare na Mlima Kenya.

“Wananchi wameshauriwa kutoendesha magari ama kutembea kwenye maji yanayoenda kwa kasi, maeneo yaliyo wazi au kukaa chini ya miti na madirisha ya chuma. Hili ni kuwazuia kupigwa na radi,” akasema Bi Stella Aura, ambaye ndiye Mkurugenzi Mkuu wa idara hiyo.

Alisema kuwa mvua hiyo inatarajiwa kuelekea katika maeneo ya kusini mashariki, kaskazini mashariki na kaskazini magharibi mwa nchi kuanzia leo hadi kesho.

Hata hivyo, kasi yake inatarajiwa kupungua kufikia Jumatatu.

Mbali na hayo, Bi Aura alionya kwamba mvua itakayonyesha katika eneo la Pwani itaandamana na pepo na mawimbi makali yenye urefu wa hadi mita mbili.