Oparanya kutetea kiwanda cha sukari

Oparanya kutetea kiwanda cha sukari

Na SHABAN MAKOKHA

GAVANA wa Kakamega, Wycliffe Oparanya ameahidi kuongoza maandamano katika kaunti hiyo kupinga watu wenye lengo la kuhujumu juhudi za kufufua kampuni ya Sukari ya Mumias.

Akizungumza Jumatatu na wanahabari, gavana huyo alisema kuwa maandamano hayo yatalenga kumtumia ujumbe Jaji Mkuu, Martha Koome kuwa wakazi wa Kakamega wanateseka kutokana na ubinafsi wa viongozi wenye nia ya kusambaratisha kampuni hiyo.

Alisema kuwa mahakama ilikuwa ikitumika vibaya na viongozi wengine ambao wamejilimbikizia mabilioni ya pesa kutokana na uagizaji wa sukari kwa gharama ya chini kutoka nchi nyingine.

Alidai kuwa baadhi ya viongozi wanatumiwa na baadhi ya watu mashuhuri kuhakikisha kiwanda hicho hakirejelei shughuli zake za kusaga miwa kama miaka ya nyuma.

Kadhalika, serikali pia iliwashutumu wanasiasa wengine wanaotoka eneo la Magharibi kutumia watu mashuhuri katika eneo hilo ili kufilisisha kiwanda hicho.

“Mwekezaji alishapewa jukumu la kuifufua kampuni hii. Hata hivyo, kuna watu waliojitokeza kisirisiri ili kusimamisha kesi ya kuifufua kampuni ya Mumias. Kwa nini mahakama inakubali watu waendelee kuteseka? Serikali inafaa kuingilia kati kuwakomesha watu ambao wanataka kufilisisha kampuni hiyo. Hii ni kwa sababu wengi walitegemea kampuni hiyo,” akasema Bw Oparanya.

Mnamo Desemba 29, mwaka jana, Mahakama ya juu ilitoa amri ya kusimamisha kampuni ya kundi la Sarrai kutoka Uganda kukodisha kampuni hiyo baada ya kampuni ya Tumaz na Tumaz ambayo ilitoa zabuni ya juu zaidi ya Sh27.6 bilioni kuenda kortini kupinga mchakato huo.

Mnamo Januari 11, mwaka huu, serikali ya Kaunti ya Kakamega, ilipata agizo la kuruhusu muungano wa Uganda kuendelea na kazi licha ya agizo lingine lililopinga hatua hiyo.Hata hivyo, mahakama ilitupilia mbali agizo hilo na kulaumu serikali ya kaunti hiyo kwa kukosa kufichua uwepo wa amri ya awali iliyositisha mchakato wa ukodishaji.

Hatua hiyo kwa mara nyingine ilitishia kusambaratisha juhudi za kufufua kampuni hiyo.Katika hafla ya kisiasa ya Bukhungu II Kakamega, kinara wa ODM, Raila Odinga, alikipendekeza kikundi cha Sarrai ili kichukue usukani katika hatua hiyo jambo lililoonekana kuwa uidhinishaji wa kampuni ya Uganda na tumaini kwa wakulima na wafanyikazi wa miwa.

Gavana Oparanya alilalamika kuwa ufufuaji wa Mumias unachukua muda mrefu licha ya juhudi zote zilizowekwa kupitia ushirikiano wa serikali ya kitaifa na kaunti pamoja na Benki ya KCB ili kubaini mwekezaji anayefaa kuchukua usukani.

“Mahakama inafaa kufutilia mbali kesi zote zinazopinga ufufuaji wa kampuni hiyo ili watu wetu wapate ajira na namna ya kujikimu.”

“Nitapambana hadi mwisho kuhakikisha kuwa kampuni ya Mumias imefufuliwa kwa kuwa waliotegemea kampuni hiyo wanaishi katika ufukara,” akasema.

  • Tags

You can share this post!

Oliech kuwa mgeni wa heshima Bukhungu tuzo za SOYA

CHARLES WASONGA: Sheria zilizoko zitumiwe kudhibiti sekta...

T L