Bambika

Oparanya: Mbona mna ishu na picha nilizopigwa na mpendwa wangu?

April 29th, 2024 2 min read

NA SINDA MATIKO

“HIVI ishu ni nini haswa kuhusu picha zangu hizo nilizopigwa na mpendwa wangu kusambazwa?”

Ndio majibu ya aliyekuwa gavana wa Kakamega, Wycliffe Ambetsa Oparanya kuhusiana na picha zake za kichokozi alizopigwa pamoja na kidosho mchanga afahamikaye kwa jina Mary Biketi.

Kwa siku kadhaa sasa, mwanasiasa huyo mkongwe mwenya miaka 68 amekuwa akitrendi mitandaoni baada ya akaunti ya Facebook ya Bi Biketi, 31, kuanza kuposti picha kadhaa akiwa na mwanasiasa huyo wakijiachia. Picha kadhaa zinawaonyesha wawili wao wakila ‘ujana’ na kujiachia kinoma noma.

Ni picha zilizoishia kuzua mdahalo mkubwa kuhusu kiini cha kuvuja kwa picha hizo hasa ikizingatiwa kuwa Oparanya ana wake wawili Priscillah na Caroline ambao wote ni wanawake wa makamu wanaotosha kuwa mama ya Biketi.

Baada ya picha hizo kuvuja, wengi waliishia kujijazia kuwa Biketi atakuwa ndio mchepuko wa Oparanya. Wapo waliohoji kuwa Biketi aliamua kuzivujisha picha hizo baada ya Oparanya kumtoka. Kuna pia tabaka la wale waliodai kuwa ni Oparanya aliyetoa baraka zake kwa picha hizo kupostiwa.

Sasa baada ya kuwa gumzo kwa takriban siku kadhaa mitandaoni, Oparanya amejitokeza na kukiri kuwa yule ni mpendwa wake na wala haelewi kwa nini picha hizo zimezua mdahalo mkubwa.

“Nimeona mtu akisambaza picha zangu, na sielewi ni kwa nini mtu atapoteza muda wake kusambaza picha kama zile ambazo ni picha safi na nzuri. Najua picha hizo zimevujishwa kwa wanahabari kutoka sehemu nilizopigia na sielewi mshawasha uliozuka kuhusiana na picha hizo nilizopigwa na mpendwa. Sasa kumezuka taarifa za uwongo kuwa mimi ni mgonjwa nimelazwa ila nipo buheri wa afya huku Mombasa kama mnionavyo ambapo nimekuwa nikikutana na watu wa jamii yangu. Nina familia kubwa ninayostahili kuilinda na kwa hiyo nawasihi wasambazaji wa taarifa hizo potovu wakome,” Oparanya kafunguka kwenye klipu ambayo imesambaa.

Ikumbukwe kuwa sio mara ya kwanza kwa Oparanya kutrendi kisa picha na demu. Mwaka jana alitrendi baada ya kuvuja kwa picha yake na demu mchanga iliyowaonyesha wakiwa kitandani faraghani.